POLISI PIC

Polisi Mkoani Kagera, Awadhi Haji

Polisi mkoani Kagera wameua watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi huku wengine wanne kukimbia na limekamata bunduki aina ya AK.47 ikiwa na magazine mbili zenye risasi 51 katika kijiji cha Nyabugombe kata ya Nyakahura wilaya ya Biharamulo.

Kamanda Polisi mkoani Kagera, Awadhi Haji amethibisha kutokea kwa tukio hilo na kusema limetokea Desemba mosi mwaka huu majira ya saa 8:00 za usiku ambapo askari polisi wamerushiana risasi na watu saba wanaodhaniwa kuwa ni majambazi  na kufanikiwa kuua watatu huku wanne wakikimbia kusikojulikana.

Haji amesema, Novemba 30, 2021 majira ya saa 3:00 usiku walipata taarifa kutoka kwa msiri kuwa, kuna watu wapatao saba wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wameonekana katika milima ya Nyabugombe wakiwa wamevaa makoti marefu ambapo walihisiwa kuwa wameficha silaha kwenye makoti hayo.

Amesema, kikosi cha kupambana na ujambazi (Ant-Robbery) walikwenda katika maeneo hayo kufanya ufuatiliaji (doria) mnamo majira ya saa 8:00 za usiku Desemba mosi, 2021 maaskari waliwaona watu hao na kuwasimamisha kwa lengo la kuwahoji ndipo watu hao walianza kuwarushia risasi askari.

Ameendelea kueleza kwamba, katika majibizano hayo askari wamefanikiwa kuwajeruhi watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kwa risasi  huku wanne wakifanikiwa kukimbia kabla hawajakamatwa na askari wamefanya upekuzi eneo hilo na kukuta silaha  moja aina ya AK.47 iliyofutika namba magazine mbili zikiwa na risasi 51 na kitambulisho kimoja chenye jina la Coyitungiye Venacie mkulima wa Muyinga nchini Burundi.

Amesema watua hao walichukuliwa na kupelekwa hospitali ya wilaya ya Biharamlo lakini walifariki muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali wakati wanaendelea  kupatiwa matibabu na kuwa miili ya watu hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hospitali ya Biharamulo, msako mkali unaendelea kwa ajili ya kuwakamata wengine waliotoroka kabla hawajakamatwa.

Wakati huohuo watu wengine wawili wanashikiliwa na jeshi hilo kwa matukio ya mauaji na kukutwa na madawa ya kulevya aina ya mairungi kilogram 10.