Mkuu wa mkoa wa Mara, Ally Hapi ametoa muda wa miezi sita uongozi wa shule ya Sekondari Morembe iliyopo manispaa ya Musoma kuandaa mpango mkakati wa kuboresha ufaulu na kuimarisha nidhamu ya wanafunzi shuleni hapo.
Hapi ametoa muda huo jana Desemba Mosi,2021 baada ya kupewa taarifa na mkuu wa shule hiyo, Kyangwe Leonard juu ya hali ya taaluma shuleni hapo ambapo mwaka jana katika matokeo ya kidato cha nne wanafunzi 60 walipata daraja sifuri kati ya wanafunzi 180 waliofanya mtihani huo.
Mkuu huyo wa shule amesema kuwa wanafunzi 88 kati ya hao waliofanya mtihani huo walipata daraja la nne huku hali ya nidhamu ya wanafunzi shuleni hapo ikielezwa kuwa ni mbaya hatua ambayo kwa namna moja ama nyingine inachangia ufaulu duni.
Mwalimu wa nidhamu shuleni hapo, Herieth Joseph amesema kuwa baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakijiunga na makundi ya uhalifu na hivyo kupelekea kuwa na utovu wa nidhamu.
Kutokana na maelezo hayo, mkuu wa mkoa alimtaka mkuu huyo wa shule kukaa na walimu wake na kupanga mikakati ya kuimarisha nidhamu na kuboresha ufaulu shuleni hapo kwa maelezo kuwa hali hiyo inachangiwa na walimu hao kutokutimiza wajibu wao.
" Hivi watoto 60 kati ya 180 wanapata divisheni ziro,88 wanapata daraja la nne halafu mnaaanza kujiteteea, kuna utovu wa nidhamu mmechukua hatua gani, hapa kuna mtendaji wa mtaa, mtendaji wa kata, mratibu elimu kata, kuna uongozi wa wilaya halafu leo mnaniambia juzi wanafunzi wawili walifanya fujo nyie kabla ya hapo mlichukua hatua gani" amehoji Hapi.
Amesema kuwa suala la nidhamu linatakiwa kusimamiwa tangu mwanafunzi anapoingia kidato cha kwanza badala ya kusubiri wafike kidato cha nne huku akisema kuwa endapo uongozi wa shule hiyo hautaboresha ufaulu shuleni hapo hatua kadhaa zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwaondoa katika nafasi zao za uongozi.
0 Comments