handeni pic

Mkuu wa wilaya ya Handeni Siriel Mchembe akipima afya jana Desemba Mosi katika viwanja vya shule ya msingi Chanika kwenye maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani. Picha na Rajabu Athumani

Mkuu wa Wilaya ya Handeni (DC), Siriel Mchembe amesema wanaume wanaongoza kwa kutokupima virusi vya Ukimwi, huku wengi wao wakitegemea wako zao ndio wakapime.

DC Mchembe amesama hayo jana Desemba Mosi, 2021 kwenye maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani akieleza kuwa katika Halmashauri ya mji maambukizi yanapungua huku kwa halmashauri ya wilaya wanaume wameonekana kukwepa kupima.

Mchembe amesema kuwa baadhi ya wanaume wanasubiri wake zao waende kliniki wakapime na wanaporudi huwauliza majibu na endapo hawana maambukizi na yeye kujiaminisha hana kitu ambacho sio sahihi.

"Katika Halmashauri ya Wilaya Handeni taarifa yao inaonyesha jumla ya wananchi waliopima ni 24,961 kati ya hao wanawake ni 12,552 na wanaume ni 12,400 hii inaonyesha wanawake ndio hujitokeza zaidi kupima afya zao kuliko wanaume" amesema Mchembe.

Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote mbili kupiga marufuku mziki wa usiku unaopigwa mitaani maarufu kama kigodoro, kwani tafiti za awali zinaonyesha kuna mambo mabaya watoto wanajifunza.

Mganga mkuu halmashauri ya Mji Handeni, Dk Feisal Said amesema katika halmashauri hiyo bado kuna unyanyasaji wa kingono ambao pia unasababisha maambukizi ya Ukimwi ambapo kwa mwaka huu kuna mimba 44 za utotoni, huku baadhi ya yao wakiwa wamekutwa wameathirika.

Kwa upande wake mkurugenzi halmashauri ya wilaya Handeni, Saitoti Stephen amewataka wananchi wa eneo hilo kujitokeza kupima bila kusubiri siku maalumu kwani kwa kufanya hivyo itawezesha Serikali kujua idadi ya walioambukizwa na kuwasaidia kupata huduma.

Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kwachanga, Rehema Rajabu amesema changamoto za kifamilia ikiwemo umasikini unaosababisha kukosekana na huduma za uhakika kwenye baadhi ya jamii, pia huchangia maambukizi ya Ukimwi.