Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Pwani, kimeridhishwa na kukamilika kwa ujenzi wa madarasa 20 yenye thamani ya milioni 400 kwa fedha za Uviko 19 ,katika Halmashauri ya wilaya ya Kibaha, huku kikisisitiza kulindwa na kusimamia thamani ya fedha za Serikali.

Aidha chama hicho ,kimebeba kilio Cha baadhi ya maeneo wanaolalamikia watoto kufuata elimu umbali mrefu ikiwemo kata ya Kawawa .

Akikagua hatua ya maendeleo ya mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa , Kilangalanga ,Disunyara na Kawawa , Mwenyekiti wa CCM Pwani , Ramadhani Maneno alisema ,wameridhishwa na hatua ya ukamilishaji wa mradi huo na ununuzi wa madawati ili kuboresha sekta ya elimu.

"Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa fedha hizi ,ambazo tumeona barabara zikijengwa, madarasa, Zahanati ,"

"Ukikopesheka kakope ,Mheshimiwa Rais tupo nyuma yake, atembee kifua mbele na CCM Pwani ,inamuunga mkono"Alieleza Maneno.

Aidha Alieleza, jambo la kufuatilia kwa mkurugenzi wa Halmashauri,katibu Tawala mkoa na Mkuu wa Mkoa ni kutatua changamoto ya baadhi ya maeneo watoto kufuata elimu umbali mrefu kama kata ya Kawawa wanaoenda Disunyara ambapo ni mbali.

Nae ofisa elimu Sekondari Halmashauri ya wilaya ya Kibaha,Fatuma Kisalazo alisema wamepokea fedha za Uviko milioni 400 kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa 20,pia milioni 200 kwa ajili ya madarasa 10 katika shule za msingi kila shule madarasa matano katika shule shikizi ili kupunguza tatizo la wanafunzi kwenda mbali kufuata elimu.

Upande wa changamoto ya upungufu wa madawati wanatarajia kutokuwepo kwani kutakuwa na madawati 791 shule za Sekondari na madawati 100 shule za msingi.

Kuhusu watoto wa eneo la Kawawa kusoma Disunyara na wazazi kuomba wahamishiwe katika madarasa yaliyo tayari kwenye kata Yao ,Fatuma alifafanua atasimama changamoto hiyo katika ngazi husika.

Diwani kata ya Kawawa,Alfred Malega aliuomba uongozi wa Chama kusaidia wanafunzi wanaofuata elimu mbali, uangaliwe uwezekano wasome kwenye Madarasa mawili yaliyo tayari .

Kaimu mkurugenzi Halmashauri ya wilaya ya Kibaha, Shukuru Lusanjala aliipongeza Serikali kuboresha sekta ya elimu na kusema anabeba maombi yaliyotolewa na wananchi na wanakwenda kuyashughulikia.