Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai amejiuzulu wadhifa wake leo Alhamisi tarehe 6 Januari 2022.

Kwa mujibu wa barua aliyomuandikia Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amesema uamuzi huo wa kuachia nafasi hiyo ameufanya kwa hiari.

"Naomba kutoa taarifa kwa umma wa Watanzania kuwa leo Tarehe 06 Januari 2022 nimeandika barua kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujiuzulu nafasi ya Spika wa bunge la Jamhuri .." imesema sehemu ya taarifa hiyo nakuongeza;

"Pia nakala yangu hiyo ya kujiuzulu nimewasilisha kwa katibu wa Bunge kwa ajili ya hatua stahiki kwa mujibu wa katiba ya nchi na sheria nyingine" amesema Ndugai kwenye taarifa yake kwa umma.

Hatua hiyo imejiri baada ya kuongezeka kwa shinikizo kutoka kwa viongozi mbali mbali ndani ya chama cha CCM kumtaka ndugai kujiuzulu baada ya majibizano kati yake na rais Samia Suluhu Hassan kuhusu serikali kuchukua mikopo ya maendeleo . Rais Samia tayari ameshajitokeza kusema kwamba kauli za Ndugai huenda zinachochewa na hofu za uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2025 .

Mapema leo Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima amemshauri Spika wa Bunge, Job Ndugai kujiuzulu nafasi hiyo kwa madai kwamba hataweza kuliongoza Bunge kwa sababu wabunge wote watakuwa upande wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Askofu Gwajima ameyasema hayo leo Alhamisi Januari 6, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akitoa maoni yake kuhusu kauli ya Spika Ndugai kuhusu mikopo aliyoitoa Desemba 28, 2021 wakati akizungumza kwenye mkutano jijini Dodoma.

Katika mkutano huo, Spika Ndugai alisema kukopa kunaongeza mzigo kwa wananchi na kwamba sasa ni wakati wa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia tozo mbalimbali zilizoanzishwa bila kutegemea mikopo.

Mbunge wa Jimbo la Mvumi Mkoa wa Dodoma (CCM), Livingstone Lusinde naye pia alikuwa amemtaka Spika wa Bunge Job Ndugai kujiuzulu kabla siku ya leo kuisha.

Akizungumza na gazeti la Mwananchi Lusinde alisema anamtaka Ndugai kuchukua hatua hiyo baada ya kujiridhisha kwa kupitia video nzima ya hotuba ya Spika Ndugai aliyoitoa hivi karibuni kwenye mkutano wa Wagogo wa Kikundi kinachofahamika kama Wanyausi.

"Napenda kusisitiza hilo na namtaka leoleo kabla ya siku kuisha awe amejiuzulu kwasababu haiwezekani mtu unaomba msamaha kwa kujitetea.. msamaha hauombwi hivyo kwa kuanza kukanusha kosa ilibidi aongee maneno machache tu" gazeti hilo limemnukuu mbunge huyo .

Baada ya ya matamshi yake kuzua mjadala nchini humo Ndugai alijitokeza katika kikao na waandishi wa habari kuomba msamaha kwa 'rais na Watanzania' lakini hatua yake hiyo haikutuliza mambo .

Akizungumza na waandishi wa habari Jumatatu Januari 3, 2021 jijini Dodoma, Job Ndugai alisema katika hotuba yake aliyoitoa hivi karibuni hakukuwa na jambo la kukashifu wala kudharau juhudi za Serikali ila alikuwa anasisitiza ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali.

Bwana Ndugai alisema kwamba mwishoni mwa mwaka uliopita alikuwa mgonjwa sana hivyo hakuweza kuwa katika nafasi ya kujitetea kwa kile kilichokuwa kinasambaa mtandaoni.

"Hali yangu ya kiafya ilikuwa si nzuri mpaka sasa mnashuhudia sauti yangu ila nataka kuweka sawa kuwa tarehe 26, mwezi Desemba nilialikwa na kikundi kimoja cha watu wa dodoma, wanaoangazia maisha ya wenyeji, kikundi hicho lengo ni ushikamano na kujenga makumbusho ya utamaduni wa watu.

Na hakukuwa kukashifu, Hapakuwa na lolote la kukashifu au kudharau juhudi zozote za serikali, katika mazungumzo yetu zaidi nilisisitiza umuhimu wa tozo na kodi."

Aliongeza kusema kuwa kama kuna mtu angeona video nzima ya kile alichozungumza, hakuna migongano ambayo ingeweza kutokea;

"Katika mazungumzo yale, baadhi ya watu wakakatakata clip ya video, wakawasilisha ujumbe nusu, ujumbe nusu ule umesababisha mjadala mkubwa katika nchi yetu, ambao mjadala umesababisha usumbufu wa hapa na pale" amesema Ndugai na kuongeza

"Hapakuwa na lolote la kukashifu wala kudharau juhudi zozote za Serikali, tunahitaji Serikali na tunaiunga mkono.

Katika mazunguzo hayo ambayo yalienda na video hiyo fupi, ninakiri kuwa mitandao ina nguvu sana na ina uwezo wa kutengeneza agenda.

Binafsi nimeumia sana kwa kauli yangu kuonekana kuwa ninapinga mkopo, mimi binafsi nina ushuhuda wa fedha hizo kutumika kujenga shule nzuri ya kiwango katika jimbo langu.' alisema wakati huo.