Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Dkt Julius Kenneth Ningu amekasirishwa na matokeo ya shule za msingi na sekondari yaliyosomwa katika kikao cha tathimini wilayani humo.


Akiongea katika kikao hicho Dkt Ningu alisema hali ya ufaulu katika shule zetu sio nzuri na jitihada za maksudi zinahitajika ili kuondokana na hali ya ufaulu duni wa wanafunzi wa wilaya ya Namtumbo.



Dkt Ningu aliwapongeza walimu wa shule zilizofanya vizuri na kuwataka kueleza sababu zilizowafanya wafanye vizuri na pia kuzitaka shule zilizofanya vibaya kueleza sababu zilizowafanya wafanye vibaya katika katika shule zao.

Baada ya kusikiliza sababu kutoka kwa walimu ambao shule zao hazijafanya vizuri mkuu wa wilaya aliwataka walimu kuziondoa alama D na E katika matokeo ya darasa la saba na darasa la nne na kuondoa daraja la 111,1v na o katika matokeo ya kidato cha nne na kuondoa daraja la 1v na 0 katika kidato cha sita.

Jacob Mbunda mratibu elimu kata ,kata ya Namtumbo alisema sababu kubwa ya wanafunzi kufeli iwe shule za msingi au sekondari ni kutozingatia masomo darasani kutokana na wazazi kutochangia chakula cha mchana kwa watoto wao hali inayosababisha wanafunzi wengi kushindwa kuhudhuria masomo Darasani ipasavyo wakati wa vipindi vya mchana

Mbunda alidai kati ya wanafunzi 246 wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Nasuli iliyopo katika kata yake wanafunzi 86 tu ndio wanaopata chakula cha mchana shuleni na kundi linalobaki linashinda na njaa hali inayosababisha kukosa utulivu darasani kwa wanafunzi hao.

Rashidi Tindwa mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kilangalanga wilayani humo alimwambia mkuu wa wilaya kuwa pamoja na wazazi kutotaka kuchangia chakula cha mchana kwa watoto wao shuleni bado kuna wazazi kuwashawishi watoto wao kutofanya vizuri mitihani yao ya kumaliza elimu ya msingi kwa kutaka kukwepa gharama ya kusomesha.

Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilaya ya Namtumbo Aggrey Mwansasu aliwataka walimu kuacha visingizio bali watumie ujuzi wao ili kuwasaidia watoto waweze kupata elimu bora na sio bora elimu.

Mwansasu alidai walimu wa zamani walikuwa na kazi mbili kwanza kuwaondoa watoto kutoka katika lugha ya kikabila na kuwaingiza katika lugha ya kufundishia yaani Kiswahili na walikuwa walimu wenye moyo wa kufundisha lakini walimu wa sasa hawana kazi hiyo watoto wengi wanajua Kiswahili ili takiwa wafaulu vizuri lakini wanamaliza darasa la saba hawajui hata kuandika wakati walimu wapo na tatizo wanaliona na wanaendelea kulifumbia macho mpaka watoto hao wanamaliza darasa la saba . 

Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo ufaulu wake umeshuka kutoka asilimia 80.443 mwaka 2020 mpaka asilimia 73.57mwaka 2021 kwa matokeo ya darasa saba na upande wa sekondari ufaulu umeshuka kutoka 86.3 kwa mwaka 2020 dhidi ya asilimia 85 matokeo ya kidato hicho mwaka 202.