TUKO KAZINI! Ndivyo unavyoweza kuelezea baada ya Shirika la Umeme Tanzania( TANESCO) kuanza mkakati wake unaofanyika nchi nzima kuhakikisha wateja walioomba umeme na kulipa Sh.27000 wanaunganishiwa umeme.


Akizungumza leo Februari 19,2022 wakati wa uzinduzi wa mkakati wa kampeni ya kuunganisha umeme kwa wateja wote waliolipa Sh.27000 kabla ya tamko la Serikali la kubadilisha bei,Msemaji Mkuu wa TANESCO Martin Mwambene amesema mkakati huo umezinduliwa leo na utaendelea hadi Machi 31 mwaka huu na wateja zaidi ya 90,000 kote nchini watafikiwa.

"Tuko kazini ndio kauli mbiu yetu TANESCO na kwa sasa tuko kwenye mkakati unaofanyika nchi nzima kwa wateja waliolipia umeme kwa Sh.27000 wanaunganishiwa umeme, Matarajio yetu hadi mwishoni mwa Machi mwaka huu tutakuwa tumemaliza, na wateja waliobakia ni 90,000,"amesema.

Amefafanua huo ni mkakati ambao unafanyika eneo kwa eneo na umeanza jana na leo Februari 19 wamezindua kampeni hiyo katika Mkoa wa Temeke kuashiria kampeni kuendelea nchi nzima,hivyo wataendelea kutoa taarifa ya kila hatua inayoendelea katika kampeni hiyo.

Ameongeza kuwa wameamua kufanya kwa maeneo maana yake wateja walioko eneo moja wote wataunganishiwa umeme hivyo hawataangalia nani amelipa mwaka jana au amelipa juzi."Tutakwenda maeneo yote na wateja ambao wamelipia wataunganishiwa umeme,tunataka kuondoa ile gharama za kwenda na kurudi, hivyo wote waliolipia umeme nchini kupitia mkakati huu tutawafikia".

Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Mkoa wa Temeke Mhandisi Satco Nombo amesema leo wako kwenye mchakato wa kuwaunganishia umeme wateja waliolipia Sh.27,000 na wanaifanya kazi hiyo kwa maeneo kwa kuhakikisha wateja waliolipiwa wanapata umeme.

Amesema katika Wilaya ya Temeke kuna timu za wafanyakazi wa TANESCO 19 kutoka Mkoa mzima n malengo yao kwa siku moja ni kuunganisha umeme kwa wateja 451."Leo kutokana na wingi wa wafanyakazi tutaunganisha kwa wateja 451 lakini kwa mipango yetu ni kwa siku nyingine ni kuunganisha umeme kati ya nyumba 250 hadi 300 na itakuwa endelevu hadi Machi mwaka huu."

Hivyo amewahakikishia wateja wote ambao wamelipia Mkoa wa Temeke hadi Machi 31 mwaka huu watakuwa wamepata umeme.Pia amesema mbali ya kuunganisha umeme wameendelea na kutoa huduma nyingine ikiwemo ya kuwepo kamati maalum inayopita kwa wateja kuchukua taarifa ili ziweke kwenye kanzi data yao.

Ameongeza mfumo huo wa kukusanya taarifa za wateja utasaidia kutafuta ufumbuzi wa changamoto ambazo zitajitokeza kwa mteja ,hivyo amewaomba wananchi kutokuwa na wasiwasi na wale wenye hofu basi wapige simu namba 0748550000 kupata uthibitisho, aidha wanaweza kuomba vitambulisho vya wakusanya taarifa hizo kutoka TANESCO.

Pia amesema TANESCO Mkoa wa Temeke wanaendelea na mchakato wa kuweka simu kadi kwa wateja wao wa njia nne ili kuweza kuwasiliana nao kirahisi hata wakiwa ofisini.


Msemaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Martin Mwambene akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 19,2022 akiwa Mkoa wa TEMEKE TANESCO ambako wamezindua kampeni ya kimkakati kutekeleza mkakati wa kuunganisha umeme kwa wateja waliolipia Sh.27000.Mkakati huo unafanyika nchi nzima



Meneja wa TANESCO Mkoa wa Temeke Mhandisi Satco Nombo (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkakati walionao wa kuunganisha umeme kwa wateja ambao wamelipa Sh.27000.

Sehemu ya wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Temeke wakijiandaa kuingia kazini kwa ajili ya kufanikisha mkakati wa kuunganishia umeme wateja wote waliolipia Sh.27000 katika Mkoa huo.






Matukio mbalimbali katika picha wakati wa kampeni ya kuunganisha umeme kwa wateja waliolipa Sh.27000.Kampeni hiyo imezinduliwa rasmi leo Mkoa wa Temeke na itaendelea kufanya mikoa yote hadi Machi 31 mwaka huu

Watumishi wa TANESCO Mkoa wa Temeke wakipanda kwenye magari kwa ajili ya kwenda kuunganisha umeme kwa wateja wao waliolipia Sh. 27000 kabla ya tamko la kubadilisha bei ikiwa ni sehemu ya mkakati wa TANESCO ulianza nchi nzima.