MAMIA ya waombolezaji katika Jiji la Dar es Salaam wakiongozwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa wameongoza ibada ya kuaga mwili wa Dk.Mwele Malecela.
Dk.Mwele ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu Mstaafu John Malecela ameagwa leo Februari 19 katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam kabla ya kupelekwa jijini Dodoma kwa ajili ya kuupumzisha mwili wake katika nyumba yake ya milele. Dk Mwele (58) aliyekuwa Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyopewa vipaumbele Shirika la Afya Duniani(WHO) alifariki dunia Februari 10 mwaka huu Mjini Geneva ,Uswiz alipokuwa akipatiwa matibabu.
Wakati wa kuaga na kutoa salamu kwa Dk.Mwele kwa wakazi wa Dar es Salaam na mikoa jirani viongozi walioko Serikali pamoja na waliostaafu wametoa salamu za rambirambi.
Akizungumza wakati akitoa salamu za rambirambi Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema enzi za uhai wake Dk.Mwele alijituma sana alipenda kuona mambo anayoyasimamia yanafanikiwa hali iliyowezesha kuipa sifa nchi yetu ya Tanzania kwa amefanya mambo mengi ya kukumbukwa.
" Sina maneno ya kuongeza zaidi ya kusema Marehemu aliitumikia nchi yake zaidi ya miaka 29, sisi sote tunapaswa kujiuliza tutaweza kufikia hayo aliyoyafanya katika kipindi cha uhai wake? Alikuwa ni mtu mwenye utu mbubwa, alikuwa karibu na watu na kupenda kuwasaidia wengine.
"Siwezi kuyasema yote lakini tuseme ya kuwa siyo tu kuyafanya tuliyoamrishwa na Mungu na kuyaacha aliyotukataza bali pia kuwatumikia watu, hili marehemu Dk. Mwele alifanikiwa," amesema Rais Mwinyi Rais wakati wa kuaga Mwili wa Dkt Mwele.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa salamu kwa niaba ya Serikali amesema Taifa la Tanzania limepoteza mtu mzuri sana ambaye ametoa mchango mkubwa sana Serikalini, ndani na nje ya nchi yetu."Kwa hiyo huzuni hii tuko pamoja na familia na tuendelee kumlilia mpendwa wetu huku tukiamini yote haya ni mapenzi ya Mungu.
"Jukumu letu ni kumuombea kwa kuwa ametangulia hatuna budi kuyaenzi yale aliyoyafanya enzi za uhai wake katika dunia hii, tunaamini ni mapenzi ya Mungu.Waziri Mkuu mstaafu mzee wetu Malecela hatuna neno zuri sana katika hili, tunakuombea uvumilivu wewe na familia yako yote, huu ni wakati mgumu lakini tupo nawe, sote kwa pamoja tunamuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi Amina"
Wakati huo huo Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba amemueleza Dk.Mwele kwa jinsi alivyofahamu ambapo amesema alikuwa mtu mwema,mkarimu na aliyependa kutumia kila aina ya busara katika kutekeleza majukumu yake.
Jaji Warioba amesema kuwa Dk. Mwele ni moja ya wasichana ambaye hakuwa muoga na anakumbuka kuna wakati Dk.Mwele alikwenda kwake kuomba ushauri kabla kabla ya kugombea urais.
"Mwele alikuwa mtu anayejiamini ,Mwele anajiamini Sana mwaka 2015 alikuja kwangu akitaka ushauri ili agombee urais nikamwambia unao uzito wa kutosha kwa kundi hilo uweze kuchukua fomu lakini akajibu baba nae ameniambia hivyo hivyo"ameema Jaji Warioba alipokuwa akizungumzia ujasiri aliokuwa nao Dk.Mwele enzi za uhai wake.
0 Comments