Miriam Fabian akiwa kwenye usukani wa gari analoliendesha wakati alipokuwa akifanya mahojiano na mwandishi wa Mwananchi.
Dar es Salaam.“Nilizoea kuwa mkarimu kwa wateja wakati nafanya biashara ya mama ntilie kwakuwa lazima uwe mchangamfu ili uwavute wateja, lakini moyo wangu umebadilika baada ya kuanza kazi ya udereva wa maroli masafa marefu.
“Kwenye nchi za wenzetu ukarimu si jambo linalozingatiwa na watu kama ilivyo kwetu, mara nyingi tunakutana na watu wenye ukatili, yaani mtu yuko tayari kufanya chochote ili apate pesa hivyo kuua si kitu cha ajabu kukabiliana nao ni lazima na wewe uwe na roho ngumu,”.
Hivyo ndivyo anavyoanza kuelezea Miriam Fabian (32) dereva wa malori ya mizigo yanayofanya safari za Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
DRC, akiwa amefanya kazi hiyo kwa miaka sita baada ya kuachana na biashara ya mama ntilie.
Katika mahojiano aliyofanya na gazeti hili Miriam anaeleza kuwa hali ya kukosekana amani na utulivu nchini DRC kunawafanya hata wageni wanaoingia katika nchi hiyo kuwa hatarini.
Kama ilivyo kwa wageni wengi, akiwa njiani ndani ya nchi hiyo huwa anakumbana na vikwazo kadha wa kadha ambavyo wakati mwingine vinamlazimu kupambana na waharifu wanaojaribu kuteka magari ili wajipatie fedha kutoka kwa madereva.
“Ukiangalia kwenye gari yangu pale mbele nimeficha mapanga, kuna muda unalazimika kuuvua ubinadamu ili uweze kujilinda maana kinyume na hapo wewe ndiye unaweza kupoteza maisha.
Mara nyingi nimekutana na matukio ya kupambana njiani, kule kuna vijana wenye fujo wanaweza kuzuia gari wakataka uwape fedha sasa hapo itategemea na namna atakavyokuja, akija kwa utulivu utazungumza naye na kumpatia kama unazo ila akija kishari ndio unalazimika kujihami kwa silaha,”
0 Comments