Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Maharage Chande (kushoto) akibadilishana mkataba wa mauziano ya umeme na kaimu Mkurugenzi wa Mgodi wa Dhahabu Geita (GGM), Wayne Loow.

 Shirika la Umeme nchini (Tanesco) limesaini mkataba wa kuuzia umeme Mgodi wa Dhahabu Geita (GGM) ambao utawezesha shirika hilo kupata Sh5 bilioni kwa mwezi.

Kwa sasa mgodi huo unatumia nishati ya mafuta ambayo kwa mwezi unalazimika kununua mafuta ya kuendeshea mitambo kwa gharama ya dola za kimarekani million tatu kwa mwezi.

Akizungumza leo Jumatatu Februari 21, 2022 wakati wa kutiliana saini mkataba huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Maharage Chande amesema mradi huo ukikamilika utondoa gharama kubwa ya wanayoingia GGM ya kununua mafuta

Amesema kupatikana kwa umeme pia kutasaidia mgodi kutunza mazingira na kuondokana na hewa ukaa wanaozalisha sasa.

Makamu wa Rais wa GGM nchini Tanzania na Ghana, Saimon Shayo amesema kwa miaka 20 wamekuwa wakitumia umeme wa kuzalisha kwa mafuta.

Amesema kwa sasa Tanesco linajenga njia ya KV 33 kwenda mgodini na mgodi utakuwa unajenga kituo cha kupoozea umeme ambavyo vyote vinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Desemba mwaka huu.

Shayo amesema pamoja na kuwa mafuta wanayotumia yanamsamaha wa kodi lakini bado gharama ya uzalishaji umeme ni kubwa kuliko umeme unaotolewa na Tanesco.