mbowe pic1

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiongoza matembezi ya mguu kwa mguu katika kata ya Kunduchi kwaajili ya kukusanya fedha za uendeshaji wa chama hicho leo Jumamosi Aprili 9, 2022.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameongoza matembezi ya mguu kwa mguu katika kata ya Kunduchi kwaajili ya kukusanya fedha za uendeshaji wa chama hicho.

 Machi 25, 2022 Makamu mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu, akiwa Ubelgiji alizindua kampeni ya ‘Joing The Chain’ yenye lengo la kuchangia chama hicho kwaajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo mkutano wa baraza kuu unaotarajiwa kufanyika Aprili 25 mwaka huu.

mbowe pic2

Akizungumza na wafanyabiashara mbalimbali leo Jumamosi Aprili 9, 2022 Mbowe amesema, wameamua kuwatembelea wananchi katika maeneo yao ya kazi, kuhamasisha wanyonge na Chadema wakiunge mkono chama na kujiunga na Join The Chain.

“Kampeni hii ni kwaajili ya kuchangia chanma chochote ulichonacho, ili kufanya ukombozi wa kweli wa nchi yetu, dhuluma zimezidi gharama za maisha zimekuwa kubwa sana na kipato cha wananchi kimezidi kupungua,”alisema Mbowe.

Amesema Serikali imezidi kustarehe hivo wanataka waonyeshe namna ya kuibadilisha Tanzania.

Mbali na Mbowe kiongozi mwingine aliyekuwepo ni pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika ambaye waligawana timu za kutembea mgu kwa mguu kwaajili ya kukusanya michango.

Hata hivyo wananchi walijitokeza kwa wingi kumshangilia Mbowe aliyekuwa ameambata na walinzi wake watatu wakiwa wamevalia sare, kwani ni kwa mara ya kwanza kwa kiongozi huyo, kujihusisha na shughuli za ujenzi wa chama toka alipotoka gerezani Machi 4 mwaka huu.

Mbowe na wenzake watatu ambao ni walinzi wake walifutiwa mashtaka ya Uhujumu Uchumi na Mahaka Kuu Division ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) kueleza kuwa hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.