Mwonekano wa Jengo la benki ya NMB, lililonusurika kulipuliwa na bomu juzi Jumamosi Septemba 17, 2022 mkoani Shinyanga. Picha na Suzy Butondo


Shinyanga. Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), wamefanikiwa kutegua bomu lililokuwa limetegwa katika Benki NMB, tawi la Shinyanga.

Bomu hilo ambalo linadaiwa kama lingelipuka lingeleta madhara makubwa kwa binadamu na mali, lilikutwa limetengwa eneo maalumu linalotumiwa na wateja wenye fedha nyingi (bulk cash) kwa ajili ya kuweka na kutoa fedha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, juzi alilithibitishia Mwananchi kutokea kwa tukio hilo akiongeza tayari mhusika mkuu anayetuhumiwa kutega bomu hilo ametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi.

Aliongeza, “Sasa Mkoa wa Shinyanga ni shwari,” alisema Kamanda Magomi alipozungumza kwa simu na gazeti hili.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema Septemba 15, 2022 saa 7 mchana, katika benki ya NMB Manonga Shinyanga, aliingia mtu anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 60 akiwa na mkoba (briefcase) wenye rangi nyeusi na koti kubwa la rangi ya kijivu.

Mmoja wa mashuhuda, Janeth Ernest, alisema mtu huyo alikuwa ameketi sehemu ya wateja wenye fedha nyingi na akiwa hapo alijifanya kama vile anajaza fomu za benki, ndipo akaliweka lile koti chini na juu yake akiweka ile briefcase.

“Inaonekana kuwa kwenye koti alilobeba kulikuwa na chupa ya Petroli maana baadae alitoa chupa hiyo na kuimwagia yale mafuta kwenye lile koti kisha kuliwasha moto kwa kiberiti na kuondoka eneo hilo,” alidai shuhuda huyo.

“Moto uliposhika kasi ndipo wafanyakazi wa benki wakashtuka na kuhangaika kuuzima,” Alidai na kuongeza kuwa baada ya kuuzima moto huo, walitoa taarifa Jeshi la Polisi na Zimamoto ambao walifika katika benki hiyo.

Mmoja wa watu waliokuwapo ndani ya benki hiyo ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini, alisema kuwa awali hawakuitilia shaka Briefcase hiyo wakidhani pengine mhusika alikuwa amebeba fedha au alikuwa amefika kutoa fedha nyingi. “Hata hivyo baada ya tukio la moto, tukaanza kuhisi kuwa pengine mkoba huo ulikuwa na vitu vya hatari zaidi ndani yake ndipo tulipoamua kupiga simu polisi na walipofika walilichukulia tukio ni la hatari.

Kulingana na vyanzo mbalimbali, Polisi walikusanya vielelezo kutoka eneo la tukio, ikiwemo sampuli ya kimiminika au petroli, vipande viwili vya mti mbichi na lile koti la kijivu na kuitoa briefcase kwa kuivuta kwa kamba hadi nje ya benki.

Inaelezwa Briefcase hiyo iliwekwa kwenye gari la polisi hadi katika kiwanja cha mpira cha Kambarage Police Barracks, ambako wataalamu wa milipuko kutoka JWTZ nao walifika kutoa msaada zaidi katika shughuli za kutegua bomu hilo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio baada ya JWTZ na Polisi kulipua bomu hilo walianza kukusanya vielelezo kwa kuvipiga picha na kuvihifadhi kwa uchunguzi zaidi.

Miongoni mwa vitu vinavyodaiwa kuwemo mbolea, vipande vya mfuko wa kiroba, tambara la shati, chanuo, mabaki ya dumu la ujazo wa lita tano, mabaki ya briefcase, pamoja na sampuli nyingine ndogondogo.

Baadhi ya watu waliokuwapo kwenye eneo la tukio waliomba uchunguzi uanze kwa kuangalia kamera za kurekodi matukio ambazo zimefungwa kwenye jengo hilo ili kupata undani zaidi wa tukio hilo.