Rais wa Uganda Yoweri Museveni amewataka raia wa Uganda kuwa macho kutokana na vitisho vya ugaidi, akiomba wageni wote wakaguliwe kabla ya kuingia katika maeneo ya ibada na sehemu za starehe.
Katika hotuba yake kwa taifa kwa njia ya televisheni Alhamisi usiku, Rais Museveni aliwataka Waganda kutoruhusu watu "wageni" kwenda makanisani na misikitini na kuwaripoti kwa polisi.
"Usiruhusu mtu yeyote usiyemfahamu kuingia kanisani au kuingia msikitini kwako.
Hakuna mgeni anayepaswa kuingia kanisani kwako, lazima apingwe, atengwe na aripotiwe polisi," alisema.
"Katika hoteli na nyumba za wageni kulala, chukua maelezo ya watu wanaokuja hapo. Hakikisha wanakuonyesha vitambulisho vyao vilivyo na picha zao,” aliongeza.
Aliwataka watu kuwa watulivu huku kukiwa na vitisho vya ugaidi vinavyohusishwa na wanamgambo wa Allied Democratic Forces (ADF), akisema vikosi vya usalama vinawawinda.

0 Comments