Wakili wa rais wa zamani wa Sudan, Omar al-Bashir, amesema mteja wake amehamishwa kutoka hospitali ambako amekuwa tangu vita vilipozuka nchini humo Aprili mwaka jana hadi "mahali salama pa kijeshi".

Mohamed al-Hassan al-Amin aliiambia tovuti ya habari ya Sudan Tribune kwamba kiongozi huyo wa zamani, pamoja na wengine wanne, wamehamishwa kutoka kwa kituo cha Matibabu baada ya huduma za afya huko "kuisha kabisa".

Bw Bashir, ambaye alikuwa amehukumiwa kwa ufisadi na alikuwa akikabiliwa na kesi ya kuongoza mapinduzi ya kijeshi mwaka wa 1989, alikuwa akipokea matibabu katika hospitali ya kijeshi katika mji wa Omdurman ambayo ilizingirwa na Wanajeshi wa Msaada wa Haraka (RSF).

Washirika wa kikanda na kimataifa wa Sudan wameshindwa kupatanisha jeshi na RSF katika muda wote wa vita ambavyo vimesababisha vifo vya takriban watu 14,000 na wengine milioni 10 kuwa wakimbizi.