Benki kubwa ya kibiashara nchini Ethiopia imewapa wateja waliotoa pesa nyingi zaidi ya walizokuwa nazo kwenye akaunti zao hadi mwisho wa wiki kuzirejesha la sivyo watakamatwa na kufunguliwa mashtaka.

Vyombo vya habari nchini viliripoti kuwa zaidi ya dola milioni 40 zilitolewa au kuhamishiwa kwa benki nyingine Jumamosi wakati wa hitilafu ya mfumo iliyodumu kwa saa kadhaa katika Benki ya Biashara ya Ethiopia (CBE) inayomilikiwa na serikali.

Katika mahojiano na BBC, Rais wa CBE Abe Sano Jumatano alisema benki hiyo imefuatilia shughuli nyingi zilizofanywa wakati wa hitilafu.

Alipoulizwa ikiwa CBE itaripoti wale ambao hawatarejesha pesa hizo kwa polisi, Bw Abe alijibu: "Ndio, ndio, kwa hakika. Tunafanya hivyo tayari".

Aliongeza kuwa benki hiyo itawachukulia hatua za kisheria wale ambao hawatakuwa wamerudisha fedha hizo “baada ya wikendi hii”.

"Hakuna njia ambayo wanaweza kutoroka kwa sababu wao ni wa kidijitali [waendeshaji pesa] na ni wateja wetu.

Tunawajua. Wanaweza kufuatiliwa na wanawajibika kisheria kwa walichokifanya," Bw Abe aliambia Newsday.

Baadhi ya wateja waliotoa pesa za ziada tayari wamezirudisha kwa benki, Bw Abe alisema.

Hata hivyo alipinga ripoti kwamba wateja walichukua $40m, akisema kiasi kilichochukuliwa kilikuwa kidogo sana lakini kitabainishwa kwa usahihi baada ya ukaguzi unaoendelea kukamilika baadaye wiki hii.

Bw Sano aliongeza kuwa ukaguzi unafanywa kwa sababu baadhi ya wateja 10,000 waliofanya miamala wakati wa hitilafu walifanya miamala halali.