Nguli wa muziki wa kufokafoka na mtayarishaji wa muziki nchini Marekani Dr. Dre ametunukiwa rasmi nyota ya Hollywood Walk of Fame siku ya Jumanne.

"Nimelelewa Compton, sikuwahi kufikiria kwamba siku moja nitakuwa na nafasi hapa katikati ya baadhi ya mashujaa wangu wa utotoni, Nitakuwa hapa siku zote" alisema Dre katika sherehe ya utambulisho.

Dr. Dre anafuata nyayo za wasanii wenzake wa rap kama Ice Cube, 2Pac na Snoop Dogg.

Mtayarishaji huyu mkongwe ambaye pia alikuwa mwanzilishi mwenza wa kikundi cha rap N.W.A alitoa albamu yake ya kwanza ya The Chronic iliyosifiwa mwaka wa 1992, ambayo ilifikia namba 3 kwenye nyimbo 200 bora za Billboard.

Wimbo wake wa kwanza alioutayarisha kushika namba moja katika chati za Billboard Hot 100 ulikuwa wa 2Pac "California Love" 1995.

Nyimbo zingine alizotayarisha ambazo zimeshika namba moja na kumpatia sifa ni "In Da Club" ya 50 Cent, "Family Affair" ya Mary J, "Crack A Bottle" ya Eminem. "No Diggity" ya BLACKstreet mnamo 1996.

Sherehe hiyo ilihudhuriwa na washirika na marafiki zake wa muda wote akiwemo Snoop Dogg, Eminem, 50 Cent, DJ Quik na Jimmy Iovine, ambao aliambatana nao kwenye sherehe hiyo ya kutambulisha nyota ya Dr. Dre.