Mahakama ya Uhispania imeamua kwamba mchezaji wa zamani wa Barcelona na Brazil Dani Alves anaweza kuachiliwa kutoka jela kwa masharti baada ya kutumikia takriban robo ya kifungo chake kwa kosa la ubakaji.

Alves, ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka minne na nusu mwezi uliopita, ataachiliwa kwa dhamana ya €1m (£853,000).

Alikuwa amezuiliwa katika kizuizi cha kabla ya kesi yake tangu Januari 2023.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 40 alipatikana na hatia ya kumbaka mwanamke katika klabu ya usiku ya Barcelona mnamo Desemba 2022.

Wakili wa mwathiriwa aliita uamuzi huo "kashfa".

Masharti ya kuachiliwa kwake ni pamoja na kugeuza pasi zake za kusafiria za Brazil na Uhispania ili asiweze kuondoka Uhispania.

Ni lazima pia afike mbele ya mahakama kila wiki.

Mahakama pia iliweka amri ya zuio, kumzuia kumkaribia mwathiriwa.

Uamuzi huo ulikuja siku moja baada ya wakili wa Alves kuomba kuachiliwa kwake kwa msingi kwamba tayari alikuwa ametumikia robo ya kifungo chake katika kizuizi cha kabla ya kesi baada ya kukamatwa.

Uamuzi huo ambao haukuwa wa kauli moja kutokana na kura iliyopinga kutoka kwa mmoja wa majaji, bado rufaa inaweza kukatwa.

Wakili wa mwathiriwa, Ester Garcia, alisema: "Kwangu mimi, ni kashfa kwamba walimwacha mtu ambaye wanajua anaweza kupata euro milioni moja na awe huru."

Mawakili wa Alves bado hawajatoa maoni yao.

Wakati wa kesi ya mwezi uliopita, waendesha mashtaka walisema Alves na rafiki yake walinunua shampeni kwa ajili ya wasichana watatu kabla ya Alves kumvuta mmoja wao kwenye eneo la VIP la klabu hiyo ya usiku lenye choo ambacho hakuwa akifahamu.

Waliteta kuwa ni wakati huu ambapo aligeuka kuwa mkali, na kumlazimisha mwanamke huyo kufanya ngono licha ya maombi yake ya mara kwa mara ya kuondoka.

Katika taarifa, mahakama ilisema kulikuwa na ushahidi zaidi ya ushuhuda wa mwathiriwa ambao ulithibitisha kuwa alibakwa.

Mwanamke huyo alisema ubakaji huo ulimsababishia "uchungu na woga", na mmoja wa marafiki zake ambaye alikuwa naye usiku huo alielezea jinsi msichana huyo wa miaka 23 alilia "bila kujizuia" baada ya kutoka bafuni.

Alves alibadilisha ushuhuda wake mara kadhaa.

Kwanza alikana kumjua mlalamishi na kudai baadaye kuwa alikutana naye chooni lakini hakuna kilichotokea kati yao.

Kisha akabadilisha ushuhuda tena, akisema kwamba walikuwa wamefanya ngono ya kukubaliana. "Sote wawili tulikuwa tukifurahia," alisema.

Alves aliichezea Barcelona zaidi ya mara 400, akishinda mataji sita ya ligi na Ligi ya Mabingwa mara tatu kwa misimu miwili akiwa na klabu hiyo. Pia alikuwa sehemu ya kikosi cha Brazil cha Kombe la Dunia la 2022.

Ameshinda mataji akichezea Sevilla, Juventus na PSG na ni miongoni mwa wachezaji wa kimataifa wa Brazil waliocheza mechi nyingi zaidi, akiwa amecheza mechi 126.