WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) umesema jitihada mbalimbali za Serikali za kuimarisha uhifadhi, uboreshaji wa miundombinu, huduma za kiutalii na utangazaji wa vivutio vya utalii ikologia ndani na nje ya nchi imeongeza idadi ya mapato ya utalii kwa kasi katika Hifadhi ya Pugu Kazimzumbwi.


Hayo yamesemwa na Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Profesa Dos Santos Silayo alipokuwa akitoa maelezo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii walipotembelea Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwe kwa lengo la kuangalia utekelezaji wa Mradi wa ustawi wa Taifa dhidi ya athari za UVIKO 19 katika msitu huo.



“Shughuli za utalii katika msitu huu zilianza 2018/19 tukiwa na watalii 533 kwa mwaka na mapato Sh. 2,465,000 kwa mwaka lakini kutokana na maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanyika kwa mwaka 2023 jumla ya watalii waliotembelea hifadhi hii walikuwa 22,491 na jumla ya mapato yaliyopatikana ni Sh.151,123,000.

Kiasi hiki ni kikubwa ukilinganisha na uchanga wa shughuli hii katika msitu huu na TFS kwa ujumla.Tunamshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuweka msukumo mkubwa kwenye suala hili kwa vitendo kwa kutuwezesha fedha za kuimarisha miundombinu ya utalii kwenye maeneo ya misitu,”amesema Profesa Silayo.

Kuhusu maboresho ya miundombinu katika msitu huo wa Hifadhi ya Mazingira Asilia Pugu,amesema ni miongoni mwa misitu 11 iliyonufaika na mradi wa kupunguza athari dhidi ya UVIKO 19. Mradi huo ulitekelezwa kama sehemu ya kuboresha miundombinu itakayokuza shughuli za utalii na kuvutia watalii kutoka maeneo mbalimbali.

Amefafanua jumla ya Sh. 579,142,176 zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika msitu huo ambapo Sh. 294,764,800 zilitengwa kwa ajili ya kufungua barabara mpya yenye urefu wa kilometa 12 kutoka Kimani-Maguruwe na ukarabati wa barabara yenye urefu wa kilometa 1 kutoka Minaki – Bwawani na ujenzi wa kilometa 7 za njia za kutembea kwa miguu kwa pamoja.

Pia Sh. 284,377,376.16 zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa lango la kuingilia lenye ofisi, kituo cha taarifa za utalii, ofisi ya malipo, kibanda cha mlinzi na vyoo huku akisisitiza utekelezaji wa mradi ulihusisha pia barabara mpya yenye urefu wa kilometa 12 kutoka Kimani – Maguruwe ambayo tayari ilifunguliwa.

“Ukarabati wa kilometa moja ya barabara kutoka Minaki – Bwawani ulifanyika.Ujenzi wa njia za kutembea kwa miguu ulifanyika kwa kiwango cha zege kwenye maeneo magumu ya njia zenye urefu wa kilometa 7 kati ya njia zenye mtandao wa kilometa 34 za kutembea kwa miguu.

“Kazi ya kufungua Barabara mpya, ukarabati wa barabara na ujenzi wa kiwango cha zege wa njia za kutembea kwa miguu ulifanyika kwa mkataba wa pamoja kwa jumla ya Sh.247,742,640.00 kwa kutumia mkandarasi Jamta Construction na kazi ilikamilika kwa mujibu wa mkataba,”amesema Profesa Silayo.

Ameongeza katika kuendelea kuimaraisha barabara hiyo mpya iliyofunguliwa, Wakala ulijenga makalavati kwa kutumia MS Controlled Blasting and Construction Co Limited ambapo line culverts 14 zilijengwa kwa Sh.126,062,350 ambazo zilikuwa ni bakaa kutoka kwenye maeneo mengine ya mradi wa UVIKO - 19 na mradi huu umekamilika.

Pia ujenzi wa kituo cha utalii cha kuingilia Pugu/Kazimzumbwi ulifanyika kwa kujenga jengo lenye ofisi ya wahifadhi, waongoza utalii, curio shop, ofisi ya malipo, chumba cha taarifa za utalii, vyoo na banda la mlinzi ambapo Sh.284,462,967.19 zilitumika.

Amewaambia wajumbe wa kamati hiyo ya Bunge kwamba miradi ya UVIKO -19 katika msitu wa Pugu Kazimzumbwi umetumia jumla la Sh.658,267,957.19 ikijumuisha na bakaa ya fedha kutoka kwenye miradi mingine.

Kuhusu manufaa ya mradi huo katika Msitu wa Pugu Kazimzumbwi ni uwepo wa barabara ya Kimani Maguruwe kilometa 12 ambayo imeanzishwa mahsusi kwa ajili ya shughuli za ulinzi wa msitu na kuongeza bidhaa za utalii kama mbio za miguu,mashindano ya mbio za baiskeli na pikipiki hifadhini.

Ameongeza pia itasaidia kuimarisha ulinzi kwa maeneo yaliyokuwa yanavamiwa hasa safu ya Kazimzumbwi (Chanika na Nyeburu).Faida nyingine ni njia za kutembea kwa miguu zinazosaidia watalii kutembea msituni kwani awali maeneo hayo yalikuwa korofi na kusababisha watalii kushindwa kufika baadhi ya maeneo yenye bidhaa za utalii.

“Ndani ya hifadhi kuna mtandao wa njia za kutembea kwa miguu zenye urefu wa jumla ya kilometa 34, ukarabati wa njia kupitia mradi wa UVIKO 19 kwa maeneo tofauti wenye jumla ya kilometa saba umefanyika na kuwa na jumla ya kilometa 25 ambazo zinafanya watalii kufikia vivutio vya utalii zilizoko ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi.

Pamoja na mradi wa kupunguza athari za UVIKO-19, Wakala kwa kutumia fedha zake za ndani na kushirikiana na wadau mbalimbali unaendelea na utekelezaji wa miradi mingine inayoendelea katika Hifadhi ya Pugu Kazimzumbwi.

Awali akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa kamati hiyo,Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Aridhi, Maliasili na Utalii Najma Giga amesema kamati imeridhishwa na matumizi ya fedha za mradi wa UVIKO-19 zilizotumika kuboresha miundimbinu ya msitu huo huku wakishauri ni vema msitu huo ukatengewa fedha kwa ajili ya kuutangaza kwani wanaamini ukiendelea kutangazwa utakuwa chanzo kikubwa cha mapato.

 

Matukio mbalimbali katika pich baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii walipotembelea Msitu wa Pugu Kazimzumbwi wilayani Kisarawe mkoani Pwani kwa lengo la kukagua utekelezaji wa mradi wa ustawi wa Taifa dhidi ya athari za UVIKO-19 katika msitu huo.