Jeshi la kijeshi la Niger limehitimisha makubaliano ya kijeshi yaliyoruhusu wafanyakazi wa Marekani kutumwa nchini humo.

Tangazo la Jumamosi lilikuja katika wiki ambayo wajumbe kutoka Washington walikuwa huko Niamey kwa mazungumzo na uongozi wa kijeshi wa nchi hiyo.

Marekani ilitumia kambi yake nchini Niger kufuatilia shughuli za kikanda za wanajihadi.

Tangazo hili la hivi punde zaidi la jeshi lililokuwa madarakani tangu Julai mwaka jana, linawadia huku likikaribia Urusi na baada ya wanajeshi wa Ufaransa kutimuliwa mwezi Desemba.

"Uwepo wa Marekani katika eneo la Jamhuri ya Niger ni kinyume cha sheria na unakiuka sheria zote za kikatiba na kidemokrasia ambazo zingehitaji watu wenye mamlaka... kushauriwa kuhusu kuwekwa kwa jeshi la kigeni katika eneo lake," msemaji wa jeshi la Niger kanali Amadou Abdramane alisema katika taarifa ya kushtumu kwenye televisheni ya taifa.

Pia alidai kuwa ujumbe wa Marekani uliishutumu Niger kwa kufanya makubaliano ya siri ya kusambaza uranium kwa Iran. Kanali Abdramane alielezea mashtaka hayo kama "ya kijinga" na "kukumbusha vita vya pili vya Iraq".

Na hatimaye, alipendekeza kuwa Marekani imeleta pingamizi kuhusu washirika ambao Niger iliwachagua. "Serikali ya Niger kwa hiyo inalaani vikali tabia ya kudharauliwa pamoja na tishio la kulipiza kisasi kutoka kwa mkuu wa ujumbe wa Marekani dhidi ya serikali na watu wa Niger," Kanali Abdramane alisema.