Utawala wa Erik ten Hag kama meneja wa Manchester United unafikia kikomo na "hakuna kurudi nyuma", amesema mshambuliaji wa zamani wa ligi ya Premia Chris Sutton.

United ilitinga fainali ya Kombe la FA Jumapili, lakini ilihitaji mikwaju ya penalti ili kuishinda Coventry, licha ya kuongoza kwa mabao 3-0 zikiwa zimesalia dakika 20 kumalizika kwa mechi hiyo katika uwanja wa Wembley.

Wako nafasi ya saba kwenye Ligi ya Premia, pointi 16 kutoka kwenye nafasi nne za juu, na walitolewa katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu huu.

"Kwa kweli sijui Ten Hag anaenda wapi baada ya msimu huu," Sutton alisema kwenye Klabu ya Jumatatu ya Usiku ya BBC Radio 5 Live.

"Ni mwisho wake sasa - hakuna njia ya kurudi baada ya hapo."

Kipa wa zamani wa Newcastle na Manchester City, Shay Given alikubali, akisema: "Hakika hatma yake haijulikani

"Haionekani kuwa hali nzuri kwake - alionekana kupotea wakati fulani kwenye mstari ambapo makocha husimama uwanjani. Kuna malalamishi mengi katika klabu kwa sasa."

Mabao kutoka kwa Scott McTominay, Harry Maguire na Bruno Fernandes yalikuwa yamewaweka Reds katika udhibiti.

Ten Hag alimtoa winga Alejandro Garnacho kabla ya bao la kwanza la Coventry, na Kobi Mainoo akatolewa muda mchache baadaye .

Wote wawili wamekuwa moto wa kuotea mbali kwa United msimu huu.

"Baada ya mechi, watu wanaangalia mabadiliko ya Ten Hag lakini hata yeye hangeweza kuona hilo wakati hali ilipokuwa mbaya zaidi.

Walikuwa wakicheza tu," alisema Sutton, ambaye alishinda Ligi ya Premia na Blackburn mnamo 1995."

Mchezo wao baada ya dakika 70 ulikuwa dalili ya jinsi Manchester United wamecheza msimu huu wote - walipoteza udhibiti."Hawakuweza kudhibiti tena mchezo na hilo limekuwa suala nyeti msimu wote."