Serikali ya Rwanda imekaribisha habari kwamba Bunge la Uingereza hatimaye lilipitisha mswada wa kuwapeleka wahamiaji haramu katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki na kusisitiza kuwa iko tayari kuwapokea wahamiaji hao.

Mahakama za Uingereza zimeweka rekodi ya haki za binadamu ya Kigali katika kipaumbele kwa kudai ulinzi zaidi kwa wale waliopelekwa huko.

Katibu wa habari wa rais na msemaji wa serikali Yolande Makolo amesema, "Tunafuraha kwamba Mswada huo umepitishwa na Bunge la Uingereza. Hata hivyo, haubadilishi kile ambacho tumekuwa tukijua kuwa ni kweli: tumefanya kazi kwa bidii katika miaka 30 iliyopita kuifanya Rwanda kuwa nchi salama kwa Wanyarwanda na vile vile, kwa watu ambao si Wanyarwanda. Hii ndiyo sababu tunaweza kutoa usalama kwa wakimbizi zaidi ya 130,000 ambao tayari wako nchini Rwanda, na kwa nini tunashirikiana na UNHCR kuwaleta wahamiaji waliokwama nchini Libya katika eneo letu ambalo ni salama. Tumejitolea kwa Ushirikiano wa Maendeleo na Uingereza na tunatarajia kuwakaribisha waliohamishiwa Rwanda."

Mahali ambapo wahamiaji wanatarajia kupelekwa pamekuwa tayari kwa karibu miaka miwili. Vyumba vimepakwa rangi mpya, ishara kwamba wako tayari kupokea wageni.

Katika mkahawa mmoja uliotembelewa na mwanahabari wa BBC, wananchi walikuwa na maoni tofauti kuhusu mpango wa wahamiaji.

Mfanyabiashara Emmanuel Kanimba, amefurahishwa na wazo hilo.

‘’Watu kutoka maeneo mbalimbali daima huleta mawazo tofauti. Na nina hakika, kwa msaada wa serikali, najua itasaidia nchi kujiendeleza zaidi na kuwawezesha watu hao kujiendeleza wenyewe.

‘’Utapata wapi ajira za watu hawa, sisi wenyewe tumehitimu masomo lakini bado hatujapata ajira. Tuko nje kutafuta kazi,’’ raia mwingine ambaye hakutaka kutambuliwa alisema.