Taifa linaloongozwa na junta limegeukia Urusi badala yake

Wanajeshi wote wa Marekani wanatazamiwa kuondoka Niger, na hivyo kumaliza jukumu lao katika mapambano dhidi ya waasi wa Kiislamu.

Viongozi wa kijeshi katika taifa hilo la Afrika Magharibi wametafuta uhusiano wa karibu na Urusi tangu kutwaa mamlaka katika mapinduzi mwaka jana.

Siku ya Ijumaa Marekani pia ilitangaza kuwa imekubali kufunga kituo chake cha ndege zisizo na rubani karibu na Agadez, katika jangwa la Sahara.

Niger iko katika eneo la Sahel barani Afrika, ambalo linachukuliwa kuwa kitovu kipya cha kimataifa cha kundi la Islamic State.

Marekani imeitegemea Niger kama ngome yake kuu katika kufuatilia shughuli za kikanda za wanamgambo wa jihadi.

Ujumbe wa Marekani utaelekea katika mji mkuu wa Niger, Niamey ndani ya siku chache, ili kupanga kuwaondoa kwa utaratibu wanajeshi wake zaidi ya 1,000.

Tangazo la Ijumaa linafuatia mazungumzo mjini Washington kati ya naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Kurt Campbell, na Waziri Mkuu wa Niger Ali Mahaman Lamine Zeine.