Nchi kadhaa za Kiafrika zimeitaka Israel ijizuie wakati baraza lake la mawaziri la vita likikutana ili kuamua iwapo italipiza kisasi dhidi ya shambulio la anga la Iran.

Iran ilisema ilifanya shambulio hilo kujibu shambulio la anga la Israel kwenye ubalozi mdogo wa Damascus tarehe 1 Aprili na kuwaua maafisa wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Shambulio hilo lilihusisha zaidi ya ndege zisizo na rubani 300 na makombora, mengi zaidi yalinaswa, jeshi la Israel lilisema.

Nigeria, Kenya, Afrika Kusini na Somalia ni nchi za Afrika ambazo zimetoa wito wa kujizuia ili kuepusha kuongezeka zaidi.

Idara ya Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini ilisema katika taarifa yake kwenye ukurasa wake wa X kwamba "wahusika wote lazima wajizuie kabisa na waepuke kitendo chochote ambacho kinaweza kuzidisha mvutano katika eneo hilo".

Rais wa Kenya William Ruto aliitaka Israel "ioneshe kujizuia kwa hali ya juu kwa kuzingatia hitaji la dharura la pande zote kuondoka ukingoni ambako kutakuwa na ugumu mkubwa wa kupona".

Alisema shambulio la Iran "linawakilisha tishio la kweli na la sasa kwa amani na usalama wa kimataifa".

Somalia ilitoa wito kwa "jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na madhubuti ili kupunguza hali hiyo na kupunguza hatari ya mzozo zaidi".

Wizara ya mambo ya nje ya Nigeria ilizitaka Israel na Iran "kutafakari juu ya dhamira ya wote ya kutatua mizozo kwa njia ya amani". Si Iran wala Israel yenye uhusiano mkubwa wa kisiasa katika Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara.