Mahakama kuu ya Huye kusini mwa Rwanda imemhukumu Beatrice Munyenyezi kifungo cha maisha jela baada ya kumkuta na hatia ya mauaji ya kimbari.

Hakimu alisema kuwa Munyenyezi mwenyewe ana jukumu kubwa katika mauaji ya kimbari na ubakaji wa wanawake na wasichana katika mji wa Butare wakati wa mauaji ya kimbari.

Beatrice Munyenyezi alirudishwa nchini Rwanda na nchi ya Marekani mwaka wa 2021 ili kufunguliwa mashtaka ya mauaji ya kimbari.

Mawakili wake walitangaza kwamba watakata rufaa kupinga uamuzi huo.

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo leo Ijumaa wahusika wote walikuwa mahakamani, mahakama ilimtia hatiani Munyenyezi kwa makosa 4 yakiwemo mauaji ya kimbari na kuchochea ubakaji wa wanawake na wasichana.

Hakimu alisema kuwa Beatrice Munyenyezi alihusika moja kwa moja katika mauaji ya baadhi ya Watutsi katika mji wa Butare ambao sasa ni mji wa Huye , akiwemo mtawa mmoja aliyeuawa na Munyenyezi mwenyewe kwa kutumia bastola baada ya kubakwa na askari kwa amri ya mshtakiwa.

Hakimu alisema kuwa maelezo ya mashahidi katika mauaji ya mtawa huyo hayana shaka.

Kadhalika Munyenyezi alishtakiwa kwa kufanya mauaji akishirikiana na mumewe Sharom Ntahobari na mama mkwe wake Pauline Nyiramasuhuko ,ambaye alikuwa Waziri wa Familia, wote wawili walifungwa Arusha nchini Tanzania baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu wa mauaji ya kimbari.

Katika utetezi wake wa mashitaka yanayomkabili katika kesi hiyo, Beatrice Munyenyezi alisema waliotoa ushahidi dhidi yake walisema uongo na ushahidi wao ulikuwa na utata.

Munyenyezi,54, alisema wakati wa mauaji ya kimbari alikuwa na ujauzito wa watoto mapacha na alikuwa na mtoto mdogo na hivyo hangeweza kujihusisha na mauaji kwa kuwa hakuwa na nguvu.

Hoja yake hiyo ilipingwa na hakimu aliyesema kwamba kuwa mjamzito hakuwezi kumzuia kutoa amri ya kuuwa na kwamba mahakama haikupata ripoti ya daktari inayothibitisha kwamba alikuwa mgonjwa au dhaifu.

Awali katika kesi hii,Munyenyezi alisema kuwa kesi yake ilichochewa kisiasa kwa sababu aliolewa katika familia iliyotiwa hatiani kwa makosa ya mauaji ya kimbari akisisitiza kwamba ‘’siyo haki kuadhibiwa kwa makosa ya wanafamilia wake’’

Mahakama ilimtia hatiani kwa makosa 4 kati ya 5 aliyoshtakiwa.

Pamoja na hayo, Hakimu alisema kuwa mmoja wa majaji 3 alikuwa na maoni "tofauti ‘’ juu ya uamuzi huo, lakini hakuwa na mengi ya kusema kuhusu hilo.

Munyenyezi alisema kuwa "hakushangazwa na uamuzi huo", huku mawakili wake wakitangaza kwamba watakata rufaa haraka iwezekanavyo.