Watu wawili wanaodaiwa kuwa majasusi wanaoshukiwa kupanga kuhujumu msaada wa kijeshi wa Ujerumani kwa Ukraine wamekamatwa katika jimbo la Bavaria kusini mwa Ujerumani.

Wanaume hao wawili, walioelezewa kuwa ni raia wawili wa Ujerumani na Urusi, walizuiliwa huko Bayreuth kwa tuhuma za ujasusi wa Urusi, waendesha mashtaka wanasema.

Dieter S, mwenye umri wa miaka 39, anashukiwa kwa msururu wa makosa ya ujasusi.

Ni pamoja na kupanga njama za mlipuko, uchomaji moto na kudumisha mawasiliano na ujasusi wa Urusi.

Pia anatuhumiwa kupigania jeshi la Urusi katika eneo la mashariki mwa Ukraine.

Mshukiwa wa pili, aliyetambulika kwa jina la Alexander J, anatuhumiwa kumsaidia tangu mwezi uliopita kutambua watu wanaoweza kufanya mashambulizi. Anatakiwa kufika mahakamani siku ya Alhamisi.

Ujerumani ni nchi ya pili kwa kutoa misaada ya kijeshi kwa Ukraine baada ya Marekani, ikitenga kiasi cha €28bn (£24bn) tangu kuanza kwa uvamizi kamili wa Urusi mwezi Februari, 2022.