Ujerumani yakabiliwa na kesi ya mauaji ya kimbari kuhusu uuzaji wa silaha kwa Israelfalse

Nicaragua imeitaka mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa kusitisha uuzaji wa silaha za Ujerumani kwa Israel mwanzoni mwa kesi ya kihistoria.

Ujerumani inashutumiwa kwa kukiuka mkataba wa mauaji ya kimbari wa Umoja wa Mataifa kwa kutuma vifaa vya kijeshi kwa Israel na kusitisha ufadhili wa shirika la misaada la Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo, Ujerumani inakanusha madai hayo na itawasilisha utetezi wake kwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) siku ya Jumanne.

Mwaka wa 2023 baadhi ya asilimia 30 ya ununuzi wa vifaa vya kijeshi vya Israeli ulitoka Ujerumani ikiwa ni jumla ya €300m ($326m; £257m).

Madai hayo yanatokea kukiwa na kesi tofauti iliyowasilishwa na Afrika Kusini mwezi Januari, ambapo majaji mjini The Hague waliiamuru Israel kuchukua "kila hatua inayowezekana" ili kuepuka vitendo vya mauaji ya halaiki.

Mahakama pia iliamuru Hamas kuwaachilia mateka wote waliochukuliwa kutoka Israel wakati wa mashambulizi yake ya tarehe 7 Oktoba mara moja.

Hata hivyo, Israel imekanusha shutuma kwamba inajihusisha na vitendo vya mauaji ya halaiki katika kampeni yake huko Gaza, na kusisitiza kuwa ina haki ya kujilinda.

Zaidi ya watu 33,000 wameuawa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza, wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas inasema, wengi wao wakiwa raia.

Gaza inakaribia kuingia katika janga la njaa, huku Oxfam ikiripoti kuwa watu 300,000 waliokwama kaskazini wameishi tangu Januari kwa wastani wa kalori 245 kwa siku.

Nicaragua inasema mauzo ya silaha ya Ujerumani kwa Israel, ambayo yalifikia dola milioni 326.5 mwaka jana - ongezeko la mara kumi mnamo 2022 - inaifanya kuwa mshiriki katika uhalifu wa kivita unaodaiwa kutekelezwa na Israeli.

Vipengele vya mifumo ya ulinzi wa anga na vifaa vya mawasiliano vilichangia mauzo mengi, kulingana na wakala wa habari wa DPA.