Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema Israel imeamua tarehe ya kufanya mashambulizi katika mji wa Rafah huko Gaza.

Serikali yake imekuwa ikiashiria nia yake ya kuanzisha operesheni ya kijeshi katika mji huo wa kusini, ambapo zaidi ya Wapalestina 1.5m wamekuwa wakijihifadhi kwa wiki kadhaa.

Bw Netanyahu alisema mashambulizi yaliyopangwa ni muhimu "kukomesha vita vya kigaidi eneo hilo".

Viongozi wa dunia wameitaka Israel kutoendelea na mpango huo kwa wiki kadhaa.

Katika uingiliaji kati wa pamoja siku ya Jumanne, viongozi wa Misri, Ufaransa na Jordan walionya Israel kuwa mashambulizi hayo yatakuwa na "matokeo ya hatari" na "kutishia kuongezeka katika kanda hiyo".

Siku ya Jumatatu, kiongozi huyo wa Israel alisema tarehe ya kuanza mashambulizi ya Rafah imekubaliwa lakini hakutoa maelezo zaidi.

Maoni ya Bw Netanyahu yanawadia huku mazungumzo kati ya Hamas na Israel kuhusu kubadilishana wafungwa na kusimamisha mapigano yakiendelea nchini Misri.