BBC Urusi, chombo huru cha Habari cha Mediazona na watu waliojitolea wamekuwa wakihesabu idadi ya wanajeshi wa Urusi waliouawa vitani tangu Februari 2022.

Makaburi mapya yalisaidia kutoa majina ya askari wengi. Timu zetu pia zilipitia ripoti huru, ripoti rasmi, magazeti na mitandao ya kijamii.

Zaidi ya wanajeshi 27,300 wa Urusi walikufa katika mwaka wa pili wa mapigano - kulingana na matokeo yetu.

Idadi jumla ya vifo – ni zaidi ya 50,000 - ni mara nane zaidi ya idadi rasmi ya vifo iliyotolewa na Moscow kwa umma mwezi Septemba 2022.

Lakini idadi halisi ya vifo inaweza kuwa kubwa zaidi.

Uchambuzi wetu haujumuishi vifo vya wanamgambo huko Donetsk inayokaliwa na Urusi na Luhansk - mashariki mwa Ukraine. Wakijumuishwa, idadi ya vifo kwa upande wa Urusi itakuwa kubwa zaidi.

Ukraine nayo haitoi mara kwa mara idadi ya vifo katika uwanja wa vita. Mwezi Februari, Rais Volodymyr Zelensky alisema wanajeshi 31,000 wa Ukraine waliuawa - lakini makadirio ya idara ya ujasusi ya Marekani, yanaonyesha idadi ni kubwa zaidi ya hiyo.


Maeneo yaliyouwa sana

dscx
Maelezo ya picha,Idadi ya vifo vya wanajeshi wa Urusi nchini Ukraine sasa imepita 50,000 - BBC inaweza kuthibitisha

Jeshi la Urusi lilikabiliwa na ongezeko kubwa la vifo mwezi Januari 2023, lilipoanza mashambulizi makubwa katika eneo la Donetsk nchini Ukraine.

Ongezeko jengine kubwa la vifo ni wakati wa msimu wa machipuko 2023, katika vita vya Bakhmut - wakati kikundi cha mamluki, Wagner, kilipoisaidia Urusi kuteka jiji hilo.

Kiongozi wa Wagner, Yevgeny Prigozhin, alikadiria hasara kwa kundi lake wakati huo kuwa ni vifo 22,000.

Urusi kuuteka mji wa Avdiivka mashariki mwa Ukraine msimu wa vuli pia kulisababisha kuongezeka kwa vifo vya wanajeshi.

Kuhesabu makaburi

FGV

CHANZO CHA PICHA,BBC/MAXAR

Maelezo ya picha,Wingi wa makaburi umeongezeka kwa kiasi kikubwa kama inavyoonekana katika picha hii.

Watu waliojitolea wanaofanya kazi na BBC na Mediazona wamekuwa wakihesabu makaburi mapya ya wanajeshi katika maeneo 70 ya kuzikia kote Urusi tangu vita kuanza.

Wingi wa makaburi umeongezeka kwa kiasi kikubwa, picha za angani zinaonyesha hviyo.

Kwa mfano, picha ya hapo juu ni makaburi ya Bogorodskoye huko Ryazan - kusini-mashariki mwa Moscow - zinaonyesha sehemu mpya kabisa ya kuzikia.

Picha na video zinaonyesha mengi ya makaburi haya ni mapya na ni ya wanajeshi na maafisa waliouawa nchini Ukraine.

BBC inakadiria angalau wapiganaji wawili kati ya watano wa Urusi waliouawa ni watu ambao hawakuwa na uhusiano wowote na jeshi la nchi hiyo kabla ya uvamizi.

‘Mwanzoni mwa uvamizi 2022, Urusi iliweza kutumia askari wake wa kawaida kufanya operesheni ngumu za kijeshi’’ anaelezea mchambuzi wa masuala ya ulinzi, Samuel Cranny-Evans wa Taasisi ya Royal United Service.

‘Lakini wengi wa wanajeshi hao wenye uzoefu kuna uwezekano wameuwawa au kujeruhiwa, na nafasi zao kuchukuliwa na watu wenye mafunzo kidogo au uzoefu wa mdogo wa kijeshi - kama vile watu wa kujitolea, raia na wafungwa.’’

Watu hawa hawawezi kufanya yale ambayo askari wa kawaida wanaweza kufanya. Hii ina maana kwamba wanapaswa kufanya mambo ambayo ni rahisi zaidi kimbinu - ambayo kwa ujumla yanaonekana ni kwenda mstari wa mbele karibu na wanajeshi wa Ukraine kwa msaada wa makombora."

Wafungwa

REF

Moscow ilimruhusu Yevgeny Prigozhin kuanza kuajiri katika magereza kuanzia Juni 2022. Wafungwa hao waliogeuka kuwa wapiganaji walipigana kama sehemu ya jeshi la kibinafsi kwa niaba ya serikali ya Urusi.

Wagner iliendelea kuajiri wafungwa hadi Februari 2023, wakati uhusiano wake na Moscow ulipoanza kuzorota. Tangu wakati huo, wizara ya ulinzi ya Urusi imeendeleza sera hiyo hiyo.

Uchambuzi wetu ulilenga majina ya wafungwa 9,000 wa gereza la Urusi ambao tunajua waliuawa kwenye mstari wa mbele.

Zaidi ya 1,000 kati yao, tulithibitisha tarehe zao za kuanza kwa mikataba yao ya kijeshi na walipouawa.

Wizara imeunda vitengo vya jeshi vinavyojulikana kama Storm platoons, ambavyo asilimia kubwa ya wapiganaji wake ni wafungwa.

Inaripotiwa kuwa vikosi hivi mara nyingi ndio hupelekwa mstari wa mbele vitani. Hivi karibuni wapiganaji wa Storm waliendesha vita vya miezi kadhaa vya kuukamata mji wa Avdiivka.

Jiji hilo liliangukia mikononi mwa Urusi wiki nane zilizopita na kuwakilisha ushindi mkubwa zaidi wa kimkakati kwa Putin tangu Bakhmut.

Wafungwa walitumwa moja kwa moja kwenye mstari wa mbele. Chini ya Wagner, wapiganaji kutoka magerezani walipewa mafunzo ya kijeshi ya wiki mbili kabla ya kuelekea kwenye uwanja wa vita.

Tulikuta baadhi ya wafungwa walio ajiriwa na wizara ya ulinzi waliuawa kwenye mstari wa mbele katika wiki mbili za kwanza za kandarasi zao.

Muda wa mafunzo hautoshi

FV

CHANZO CHA PICHA,REUTERS

Maelezo ya picha,Yevgeny Prigozhin, aliyekuwa kiongozi wa kundi la Wagner kabla ya kifo chake

BBC imezungumza na familia za wafungwa waliofariki - na wanajeshi ambao bado wako hai - walituambia mafunzo ya kijeshi yanayotolewa kwa walioajiriwa na wizara ya ulinzi hayatoshi.

Mjane mmoja alituambia mume wake alitia saini mkataba tarehe 8 Aprili mwaka jana - na alipelekwa mstari wa mbele siku tatu baadaye.

"Nilikuwa na uhakika kungekuwa na wiki chache za mafunzo. Na hakutakuwa na kitu cha kuogopa hadi angalau mwisho wa Aprili."

Anasema alisubiri kusikia kutoka kwa mumewe - lakini akagundua ameuawa tarehe 21 Aprili.

Mama mwingine anasema aligundua mumewe alitolewa gerezani na kupelekwa uwanja wa vita, alijua baada ya kujaribu kuwasiliana naye kuhusu kifo cha mtoto wao wa kiume, ambaye pia alikuwa akipigana.

Mwanamke huyo, tunamwita Alfiya, anasema mwanawe Vadim mwenye umri wa miaka 25 - baba wa mapacha - hakuwahi kushika silaha kabla.

Anasema hakuweza kumwambia mumewe Alexander kuhusu kifo cha mtoto wao kwa sababu alikuwa amechukuliwa kwenda kupigana. Aligundua mumewe amekwenda vitani kupitia simu kutoka kwa mfungwa mwingine.

Alexander alikulia Ukraine na alikuwa na familia huko. Miezi saba baada ya kifo cha mwanawe, Alfiya aliarifiwa Alexander pia ameuawa.

Uwe tayari kufa

FD
Maelezo ya picha,Makaburi ya wanajeshi huko Bakinskaya Kusini mwa Urusi

Wakati wa kufanya kazi na Wagner, wafungwa walipewa kandarasi kwa miezi sita. Ikiwa utanusurika utapewa uhuru wako.

Lakini, tangu Septemba iliyopita, chini ya wizara ya ulinzi, wafungwa walioandikishwa lazima wapigane hadi wafe au vita viishe.

BBC imesikia habari za wafungwa wakiomba jamaa zao kuwasaidia kununua sare na buti zinazofaa. Pia kumekuwa na ripoti za wafungwa kutumwa kupigana bila vifaa vya kutosha vya matibabu.

"Baadhi ya Askari walikuwa na bunduki ambazo hazikufaa kwa mapigano," anaandika mwanablogu Vladimir Grubnik na muungaji mkono wa vita hivyo, kwenye chaneli yake ya Telegram.

Grubnik anaishi mashariki mwa Ukraine inayokaliwa na Urusi - anadai makamanda walipogundua baadhi ya bunduki zimevunjika walisema haiwezekani kubadilishwa.

"Ukijiandikisha sasa, uwe tayari kufa," anasema Sergei, katika jukwaa la mtandaoni la wapiganaji wa Storm na jamaa zao.

Anadai yeye ni mfungwa wa zamani ambaye amekuwa akipigana katika kitengo cha Storm tangu Oktoba.

Mwanachama mwingine wa jukwaa hilo anasema alijiunga na kikosi cha Storm cha askari 100 miezi mitano iliyopita na sasa ni mmoja wa askari 38 tu ambao bado wako hai.