Maandamano ya kupinga vita huko Gaza yameenea kutoka Columbia na Yale hadi vyuo vikuu vingine nchini Marekani huku maafisa wakihangaika kukabiliana nayo.

Siku ya Jumatatu usiku, polisi walitawanya maandamano katika Chuo Kikuu cha New York na kukamata watu kadhaa.

Wanafunzi wengi walikamatwa huko Yale mapema siku hiyo wakati Columbia ilipositisha masomo ya ana kwa ana darasani.

Maandamano kama hayo yameibuka huko Berkeley, MIT na vyuo vingine kote nchini humo.

Maandamano na mijadala mikali kuhusu vita vya Israel na Gaza na uhuru wa kujieleza vimetikisa vyuo vikuu vya Marekani tangu kutokea kwa shambulio la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba.

Takriban Waisrael na raia wa wageni 1,200 - waliuawa na wengine 253 walirejeshwa Gaza kama mateka, kulingana na hesabu za Israel.

Israel ilijibu kwa kuanzisha vita vyake vikali zaidi kuwahi kutokea huko Gaza kwa malengo ya kuangamiza Hamas na kuwakomboa mateka.

Zaidi ya Wapalestina 34,000 huko Gaza - wengi wao wakiwa watoto na wanawake - wameuawa katika mzozo huo, wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas inasema.

Nchini Marekani, wanafunzi wa pande zote mbili wanasema kumekuwa na ongezeko la matukio ya chuki dhidi ya Wayahudi na Uislamu.

Alipoulizwa kuhusu maandamano ya chuo hicho siku ya Jumatatu, Rais Joe Biden alisema alilaani "maandamano ya chuki dhidi ya Wayahudi" pamoja na "wale ambao hawaelewi kinachoendelea na Wapalestina".