Takriban Wapalestina 12 wameuawa katika shambulizi la anga la Israeli dhidi ya shule inayohifadhi watu waliokimbia makazi yao katika jiji la Gaza, mamlaka ya Ulinzi wa Raia inayosimamiwa na Hamas imesema.

Msemaji alisema waokoaji walikuwa na wakati mgumu kupata watu kadhaa waliotoweka wanaoaminika kukwama chini ya vifusi katika shule ya Mustafa Hafez, kitongoji cha Rimal magharibi.

Jeshi la Israeli limesema lililenga kamandi na kituo cha udhibiti cha Hamas ndani ya shule hiyo, na kwamba imechukua hatua za kupunguza hatari ya kuwadhuru raia.

Hapo awali, ilitangaza kwamba wanajeshi walikuwa wamepata miili sita ya mateka wa Israeli waliokuwa wakishikiliwa katika eneo la Khan Younis.

Watu hao walikuwa miongoni mwa watu 251 waliotekwa nyara na wapiganaji wanaoongozwa na Hamas katika mashambulizi ya Oktoba 7 kusini mwa Israeli mwaka jana, wakati takriban watu 1,200 pia waliuawa.

Israeli ilianzisha operesheni ya anga na ardhini kumaliza kundi la Hamas katika hatua ya kujibu shambulizi walilotekeleza, ambapo zaidi ya watu 40,170 wameuawa huko Gaza, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayosimamiwa na Hamas