Hillary Clinton amesema kuwa ana matumaini kwamba Kamala Harris hatimaye ataweza "kuweka historia mpya" nchini Marekani kwa kuwa rais wa kwanza mwanamke.

Akizungumza katika kongamano la kitaifa la chama cha Democratic Bi Clinton alisema kuwa yeye binafsi ameweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kushinda uteuzi wa chama kikuu kuwania tiketi ya urais.

“Mmoja wetu akiondoa kizuizi, ametufungulia njia sisi sote,” alisema, akirejelea hotuba yake miaka minane iliyopita.

Lakini wakati azma yake ya kuwania urais mwaka 2016 ilikuwa ya kihistoria, hatimaye iliishia kushindwa katika uchaguzi na Donald Trump.

Nyakati zimebadilika tangu Bi Clinton agombee urais wa Marekani, kulingana na wajumbe kadhaa wa kike na wanasiasa wanaohudhuria Kongamano la mwaka huu mjini Chicago.

Wakati wake Bi Clinton alitumia jinsia yake kuwa sehemu kuu ya kampeni - hatua ambayo Bi Harris amechagua kuikwepa.