Madaktari katika hospitali za umma nchini Nigeria wameanza mgomo wa siku saba nchini kote wakitaka mwenzao, Dk Ganiyat Popoola, ambaye amekuwa akishikiliwa na watekaji nyara kwa muda wa miezi minane.

Mama huyo wa watoto watano alichukuliwa kutoka nyumbani kwake katikati ya usiku wa Disemba 27 pamoja na mumewe na mpwa wake.

Mumewe aliachiliwa mnamo Machi baada ya fidia kuripotiwa kulipwa lakini watekaji nyara walimshikilia daktari wa macho na jamaa yake.

Madaktari hao wanasema hata hawatatoa huduma ya dharura wakati wa mgomo huo.

Dk.Popoola anafanya kazi katika hospitali ya Kituo cha Kitaifa cha Macho huko Kaduna, kaskazini-magharibi mwa Nigeria, na anaishi katika sehemu rasmi zinazotolewa na hospitali hiyo.

Hospitali hiyo ni mojawapo ya hospitali kubwa za macho nchini.

Wataalamu wanasema eneo la hospitali hiyo nje kidogo ya jiji la Kaduna linaifanya kuwa shabaha rahisi kwa watekaji nyara. Mnamo 2021, wanafunzi kadhaa walichukuliwa kutoka chuo cha karibu cha misitu.

Dk.Taiwo Shittu wa Hospitali ya Kufundisha ya Chuo Kikuu cha Lagos alisema kilichompata Dkt.Popoola kinaweza kumpata mtu yeyote.

"Tunataka mamlaka kuchukua hatua haraka, hii imeendelea kwa muda mrefu sana," alisema kwenye video kwenye mtandao wa kijamii.

Madaktari wanahisi vyombo vya usalama havifanyi vya kutosha kuhakikisha aachiliwe. Watekaji nyara wanaomba 40m naira (£19,000; $25,000) kwa ajili ya uhuru wao. Ingawa sheria tata inayoharamisha malipo ya fidia ilianza kutumika mwaka wa 2022, bado mara nyingi hulipwa na watu wa ukoo wanaotamani kuwaachilia wapendwa wao.

Sheria ina adhabu ya kifungo jela cha takribani miaka 15 kwa yeyote atakayelipa fidia, ingawa hakuna mtu ambaye amehukumiwa.