Mamlaka nchini Tanzania zimeteketeza ekari 1,165 za mashamba ya bangi na kukamata kilogramu 102 za mbegu za bangi mkoani Morogoro, mashariki mwa nchi hiyo.

Aidha, katika operesheni maalum kwenye mkoa huo, mamlaka iliwakamata watu sita waliokuwa na kilogramu 342 za bangi.

Akizungumza leo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo amesema mashamba ya bangi yaliyoteketezwa yamelimwa kwenye eneo la akiba la hifadhi ya Taifa Mikumi.

Kamishna huyo alisema, “Uharibifu mkubwa sana wa mazingira umefanyika katika eneo hili ambapo miti imekatwa ili kupata eneo la kulima bangi na hivyo kuharibu uoto wa asili…

“Pia uharibifu uliofanyika katika eneo la akiba la Mikumi unaharibu ikolojia ya eneo hilo na kufanya uharibifu mkubwa wa uoto wa asili na ikizingatiwa mito hiyo inatiririsha maji katika bwawa la Mwalimu Nyerere linalotegemewa kwa uzalishaji wa umeme,” alisema Lyimo.

Lyimo pia amewaomba wananchi wa mkoa wa Morogoro na mikoa mingine kushirikiana na Mamlaka kupiga vita kilimo cha bangi na aina nyingne za dawa za kulevya.

Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 2022 iliandaliwa na DCEA ilitaja Morogoro, Arusha, Iringa, Ruvuma, Manyara na Mara kuongoza kwa kilimo cha bangi.