Maji kwenye sehemu za ufuo wa Mediterania wa Gaza yameanza kubadilika rangi na kuwa ya hudhurungi huku wataalamu wa afya wakionya kuhusu kuenea kwa maji taka na magonjwa katika eneo hilo.

Picha za satelaiti, zilizochambuliwa na BBC idhaa ya Kiarabu, zinaonesha kile kinachoonekana kuwa ni utiririshaji mkubwa wa maji taka kwenye pwani ya Deir al-Balah.

Afisa mmoja wa eneo hilo aliiambia BBC kwamba watu waliokimbia makazi yao katika kambi za karibu wanapeleka maji taka yao moja kwa moja baharini.

"Ni kwa sababu ya ongezeko la idadi ya watu waliokimbia makazi yao na wengi wanaunganisha mabomba yao wenyewe kwenye mfumo wa mifereji ya maji ya mvua," alisema Abu Yazan Ismael Sarsour, mkuu wa kamati ya dharura ya Deir al-Balah.

Wim Zwijnenburg, mtaalamu wa mazingira kutoka shirika la Pax for Peace, alithibitisha kuwa maji machafu yalionekana kuelekea baharini kutoka kwenye kambi za karibu zilizojaa watu, baada ya kuchunguza picha za satelaiti.

Haijabainika ikiwa uchafuzi wa mazingira wa pwani bado unaongezeka kwani picha za hivi karibuni zaidi za satelaiti hazipatikani.

Mashambulizi makali ya Israel yamesababisha kuporomoka kwa miundombinu ya usimamizi wa maji taka Gaza, ripoti ya mazingira ya Umoja wa Mataifa ilihitimishwa mwezi Juni.

Chombo cha wizara ya ulinzi ya Israel kinachosimamia sera za maeneo ya Palestina, Cogat, kiliiambia BBC Kiarabu kwamba kikosi kazi kilichojitolea cha kibinadamu kimechukua hatua kuboresha mfumo wa maji taka huko Gaza.

Katika miezi ya hivi karibuni, Cogat iliratibu urejeshaji wa visima vya maji na vifaa vya kuondoa chumvi, pamoja na upanuzi wa mabomba ya maji huko Gaza, kulingana na taarifa yake.