Jeshi la Polisi nchini Tanzania linawashikilia watu wanne akiwemo mganga wa kienyeji kwa kuhusika na mauaji ya watu 10 huku vifo vyao vikihusishwa na imani za kishirikina.

Aidha baadhi ya watu waliuwawa kwa kunyongwa, kuzikwa wakiwa hai na mwingine kuchomwa moto.

Ilibainika kuwa miili mitatu ilikutwa imezikwa nyumbani kwa mganga huyo katika mkoa wa Singida wakati miili mingine sita ilizikwa wilayani Chemba (Dodoma) na mmoja kutupwa kwenye pori la akiba la Swangaswanga, Dodoma.

Katika taarifa iliyotolewa na Msemaji wa jeshi hilo, David Misime miili 9 kati ya 10 ilizikwa kwa kukalishwa kwenye shimo huku kitendo hicho kikiashiria imani za kishirikina.

Misime alisema, matukio hayo yote yaliongozwa na mganga huyo ambapo baada ya uchunguzi kuhusu vifo vya watu watatu ambao miili yao ilifukuliwa nyumbani kwake, mganga huyo alilionyesha jeshi hilo alipozika miili mingine sita baada ya kutekeleza mauaji.

Alibainisha kuwa waliothibitika kuuwawa baadhi walinyongwa, kuzikwa wakiwa hai na mwengine kuchomwa moto.

Hata hivyo, miongoni mwa miili sita iliyoripotiwa kuzikwa Dodoma, miwili ilikuwa ni ya watoto waliouwawa na kuzikwa kwenye zizi la mifugo katika kipindi cha mwezi Machi na Juni mwaka jana ambapo mmoja wao alikuwa mtoto wa mganga huyo wa kienyeji.

Jeshi hilo limesema linaendelea na uchunguzi wa mlolongo wa matukio hayo katika mkoa wa Singida na Dodoma.

Sambamba wanafuatilia wengine wanotekeleza uhalifu kama huo.