Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema atawasilisha mpango kwa Marekani kuhusu jinsi anavyodhamiria kumaliza vita na Urusi.

Zelensky, ambaye amezungumza na waandishi wa habari kuadhimisha siku ya uhuru wa Ukraine ambayo ilikuwa Jumamosi, anasema atawasilisha mpango huo kwa wagombea urais Kamala Harris na Donald Trump, pamoja na Rais wa sasa Joe Biden.

Mpango huo utajumuisha hatua katika nyanja za kidiplomasia na kiuchumi, anasema, tofauti na uvamizi wa Ukraine huko Kursk, ambao pia umekuwa sehemu ya mkakati wa kuifanya Moscow kuanza mazungumzo ya amani.

Zelensky pia anauambia mkutano wa wanahabari mjini Kyiv kwamba Ukraine ilifanya jaribio la kwanza la kombora la balestiki lililotengenezwa nchini humo.

Ukraine tayari imetumia baadhi ya makombora ya balistiki dhidi ya Urusi ambayo yalitolewa na Marekani.