Rais Volodymyr Zelensky amemfuta kazi kamanda wa kikosi cha anga cha Ukraine huku kukiwa na mjadala kuhusu kuanguka kwa ndege mpya ya kivita ya F-16 yenye thamani kubwa nchini humo.

Bw Zelensky hakutaja sababu ya kumfukuza kazi Luteni Jenerali Mykola Oleshchuk, lakini alisema ana jukumu la "kuwatunza wapiganaji wetu wote".

Ndege hiyo aina ya F-16 iliyotengenezwa Marekani - mojawapo ya ndege kadhaa zilizotolewa mapema mwezi huu na washirika wa Magharibi wa Ukraine - ilianguka Jumatatu, na kumuua rubani.

Ingawa ilitokea wakati wa msururu wa makombora ya Urusi, Ukraine ilisema chanzo cha ajali hiyo haikuwa matokeo ya moja kwa moja ya shambulio la adui, na Luteni Jenerali Oleshchuk alijipata akiwa matatani na baadhi ya wanasiasa kuhusu nani alaumiwe kwa hasara hiyo.