Ujerumani imewaondoa wanajeshi wake wa mwisho waliosalia katika eneo linalosimamiwa na Niger, hatua inayoashiria mwisho wa operesheni zake huko Sahel.

Kuondoka kwao kulikamilika siku ya Ijumaa na kutangazwa na maafisa waandamizi wa jeshi la Ujerumani na Niger.

Wanajeshi 60 wa Ujerumani na tani 146 za vifaa vilivyosafirishwa na ndege tano za mizigo zilitua Ujerumani Ijumaa usiku.

Mnamo mwezi Mei, Niger ilikubali kuruhusu wanajeshi wa Ujerumani kuendelea kuendesha shughuli zao katika kambi yao ya wana anga huko Niamey hadi Agosti 31.

Mazungumzo yaligonga mwamba kati ya pande zote mbili baada ya Niger kushindwa kuhakikisha kwamba majeshi ya Ujerumani nchini humo yangenufaika na kinga dhidi ya kufunguliwa mashtaka.

"Kujiondoa kwao hakuashirii mwisho wa ushirikiano wa kijeshi kati ya Niger na Ujerumani," maafisa kutoka nchi zote mbili walisema katika taarifa ya pamoja iliyosomwa, wakionyesha kujitolea kwao kudumisha uhusiano wa kijeshi.

Hata hivyo, kauli hiyo ni tofauti kabisa na ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock, ambaye alisema mwezi Julai kuwa hawawezi tena kushirikiana na Niger kwa sababu ya kukosekana kwa uaminifu.

Ujerumani ilianza operesheni katika kambi yake ya wanajeshi wa anga huko Niamey mwaka wa 2016, na ilikuwa na wanajeshi takriban 3,200.

Berlin pia ilichangia katika vita dhidi ya waasi katika nchi jirani ya Mali, kama sehemu ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani ambao ulilazimika kutamatisha shighuli zake mwaka jana.