MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeendelea kuimarisha doria za muitikio wa haraka na matumizi ya mabomu baridi kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu.

Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mabula Misungwi Nyanda amesema hayo leo Septemba 6, 2024 katika hafla ya ugawaji vifaa yakiwemo mabomu baridi 2,567 kwa makamanda wa kanda 7 za uhifadhi za mamlaka hiyo kwa ajili ya kuendelea kukabiliana na changamoto hizo.

Mabula amewataka makamanda wa kanda hizo kuhakikisha askari wa uhifadhi na askari wa vijiji wanapatiwa mafunzo stahiki ya kutumia mabomu baridi na wahakikishe kuwa mabomu hayatumiwi na wananchi.

Pia makamanda wa kanda za uhifadhi wamekabidhiwa vitendea kazi vingine ikiwemo vuvuzela (548), tochi (1,451) na filimbi (500).

SOMA: Wizara ya utalii yadhibiti wanyamapori wakali

Amesema kuwa vifaa hivyo visivyo na mlipuko vitagawiwa kwa wananchi kwa ajili ya kusaidia kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu maeneo yao zikiwa ni hatua za awali.

“Tunaendelea piakutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kuepukana na kukabiliana na madhara yaletwayo na wanyamapori wakali,” amesema Kamishna Mabula.

Amesema mamlaka itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti wanyama wakali ikiwemo kuimarisha doria za muitikio wa haraka, kushirikisha askari wa vijiji 184, kujenga vituo vya udhibiti, kununua vitendea kazi ikiwemo magari, ndege nyuki, pikipiki na vilipuzi .

Katika hatua nyingine amesema kwa mwaka wa fedha 2024/ 2025, TAWA imepanga kuendelea kujenga vizimba vya kudhibiti mamba na kuchimba mabwawa.

Mabula ametaja eneo lingine ni kununua ndege nyuki zenye uwezo wa kumwaga maji yenye pilipili kwa ajili ya kufukuza tembo kwenye maeneo ya wananchi.

Kamishna Mabula ametoa rai kwa wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano kwa wahifadhi wa wanyamapori kwa kuzingatia ushauri wanaopewa na wataalamu ikiwemo kuacha kufanya shughuli za kibinadamu maeneo ya shoroba. Mabula amewataka kuacha matembezi ya usiku yasiyo na lazima na kuchukua tahadhari wanapofanya shughuli za binadamu katika mito, mabwawa na maziwa.

 

Kwa upande wake, Kamanda wa Kanda ya Kusini Mashariki, Abraham Jullu, kwa niaba ya makamanda wa kanda za uhifadhi ametoa shukrani kwa kukabidhiwa vitendea kazi hivyo.

Jullu amesema vitendea kazi hivyo vitasaidia katika kupunguza madhara yatokanayo na mnyamapori tembo kwa kuwa imebainika na kudhihirisha kuwa baada ya kuanza kutumia mabomu baridi visa vya wanyamapori hao vemupunga kwa kiwango kikubwa.