WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassaan anamatumaini makubwa kuwa timu ya taifa ya mpira wa miguu ‘Taifa Stars’  itafanya vizuri kwenye michezo yote miwili ya kufuzu mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON).

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo alipotembelea timu hiyo kwenye uwanja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jijini Dar es Salaam inakofanya mazoezi.

Akiwa uwanjani hapo, Majaliwa amezungumza na wachezaji, benchi la ufundi pamoja na viongozi.

“Kila mmoja aone ana jukumu kubwa, kwako wewe mwenyewe na kwa nchi yako, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anawatakia kila la kheri na alichofanya ametoa usafiri wa uhakika wa ndege itakayowapeleka nchini Congo kwa ajili ya mchezo wa Oktoba 10, 2024, hili ni jambo kubwa,” amesema Majaliwa.

SOMA: Mbwana Samatta arejeshwa Stars


Majaliwa amesema kwa jitihada za Rais Samia amefanikiwa kushawishi mashirikisho ya mpira wa miguu ya Afrika na FIFA ili kuiona Tanzania ni nchi ambayo imeamua kuboresha viwango vya michezo ikiwemo mpira wa miguu. “Tumeanza kuona heshima tunayoipata ya kuwa wenyeji wa baadhi ya mashindano ikiwemo CHAN.”

Kwa upande wake, Nahodha wa timu hiyo Mohammed Hussein “Tshabalala” amemshukuru Rais  Samia kwa kuwezesha kupatikana kwa usafiri wa ndege kwa ajili ya mchezo dhidi ya Congo.