MTWARA: WAKATI msimu wa uuzaji wa korosho ukikaribia kufunguliwa, Mamlaka ya Bandari ya Mtwara imesema meli tatu na kontena zaidi ya 1000 zimeshawasili bandarini hapo kwa ajili ya kuhudumia mizigo ya korosho zinatakazosafirishwa kwenda nje ya nchi.

“Hadi sasa hivi tumeshapokea meli tatu za korosho na kontena zaidi ya 1000,” Meneja wa Bandari wa Bandari Fernard Nyathi amesema na kuongeza kuwa makasha ya kubeba korosho yamewasili mapema tofauti na msimu wa mwaka jana.

Nyathi amesema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja. 

Amesema kuna meli nyingine ambayo inatarajia kuleta kontena nyingine 600, ili kuhudumia korosho kutoka mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.

Akizungumzia wiki ya huduma kwa wateja, Nyathi amesema Bandari ya Mtwara imejipanga kuwahudumia wateja wao ambapo watawatembelea wateja wao wote, na kuwa na dawati la huduma kwa wateja.

“Tutafanya customer visit, kutembelea wateja wetu wote ambao wanapatikana hapa Kusini, tutakuwa na dawati la huduma la wateja , tutarudisha shukrani zetu kwa wateja wetu,” amesema.