HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro imetenga Sh milioni  827 kwa ajili ya mikopo ya asilimia10 kwa wananchi walio kwenye vikundi vya ujasiriamali vya vijana, wanawake na wenye ulemavu ili waweze kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Mkurugenzi wa Malmashauri Manispaa hiyo, Emmanuel Mkongo  amesema hayo wakati wa kuhitimishwa mbio za pole zilizoandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro ambazo zililenga kuhamasisha masuala ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Mkongo amesema kuanzia Oktoba 3, mwaka huu taarifa imetolewa kwa wananchi  ya kuanza utaratibu  mpya wa utoaji mikopo ya makundi ya wanawake,vijana na wenye ulemavu .

“Tumeshaanza rasmi kwa makundi haya  na sasa yajitokeze  kuomba mikopo hii hadi kufikia  Oktoba 15, mwaka huu,” amesema Mkongo.

Mkongo amesema mikopo hiyo kulingana na maelekezo maapya inaombwa kwenye mfumo rasmi ambao ulishaandaliwa , na  kwamba vikundi  vinapaswa kujiandikisha kwenye maeneo yao ya kata husika.

“Mikopo inachakatwa na yale maandiko, na miradi yao inafanyiwa uchambuzi na wakati mwingine  Maofisa Maendeleo ya Jamii wa zile kamati za mikopo watatembelea  na kujiridhisha na hiyo miradi “ amesema Mkongo.

Mkongo amesema kuanzia Oktoba hadi Novemba mwaka huu , manispaa inatarajia kuchakata na kutoa fedha kwa zaidi ya Sh milioni 800.

“ Kitu cha msingi ni wale wenye sifa kuomba kwenye mfumo na wakishaomba utaratibu utafanyika ,na wale  wenye kupata changamoto ya kutumia mifumo  tunawashauri wafike maeneo yao ya kata ama  kwenye Ofisi kuu ya halmashauri ili wapate msaada” amesema  Mkongo.

Kwa  upande wake  Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala alisema serikali imeboresha upatikanaji na utoaji  wa mikopo ya asilimia 10 baada ya kusitiwa kwa sababu mahususi  kutokana na kwamba  wale waliokuwa na sifa walikuwa hawapati mikopo hiyo.

Kilakala amesema  kulikuwepo na baadhi ya watumishi walituhumiwa kutengeneza vikundi hewa  ambavyo haviwanufaishi  wananchi .