DODOMA: SERIKALI imetenga sh bilioni 300 kwa mwaka wa fedha 2024/25 ili kugharamia ruzuku ya mbolea kwa wakulima.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli wakati akifungua Kongamano la Kwanza la Mbolea linalofanyika Oktoba 11 na 12 katika Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.

Kongamano hilo lililoratibiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) limehusisha uzinduzi wa Mkakati wa Mbolea utakaosaidia katika uendelezaji wa tasnia ya mbolea nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Katibu Mkuu Mweli amesema serikali imeendelea kuimarisha sekta ya kilimo nchini kwa kuwezesha utoaji wa ruzuku ya mbolea kwa misimu mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2022/23 hadi 2024/25.

Kongamano hilo la siku mbili ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani inayoadhimishwa Oktoba 13 kila mwaka ambapo mwaka huu inaadhimishwa nchini kwa mara ya sita.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka 2024/25 ni ‘Tuongee Mbolea, Kilimo ni Mbolea’, yakiwa yamewakutanisha wadau mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa mbolea kutoka ndani na nje ya nchi.

Aidha, Katibu Mkuu amezipongeza kampuni za ndani zinazozalisha mbolea kuendelea kuzalisha mbolea kwa wingi na ametoa rai kwa wawekezaji mbalimbali kuja kuzalisha mbolea nchini na kuhakikisha matumizi ya mbolea yana akisi na afya ya udongo ili Tanzania ifikie malengo ya kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa mbolea katika Mataifa mengine Barani Afrika.

Wadau hao ni pamoja na watunga sera, wazalishaji wa mbolea, waingizaji na wafanyabiashara wa mbolea, watafiti, wanazuoni, taasisi za fedha, wadau wa maendeleo, wataalam wa kilimo na wakulima.

Kongamano hilo limehudhuriwa pia na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara Kilimo, Mifugo na Uvuvi; wakiwemo wadau wa maendeleo pamoja na wawakilishi kutoka Mataifa mbalimbali.

Katika kongamano hilo, washiriki watajadili na kuazimia masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya Tasnia ya Mbolea na Sekta ya Kilimo kwa ujumla.