WANAFUNZI wa vyuo vikuu na kati wameshauriwa kutotumika kwa namna yoyote ile kutimiza lengo la mtu au kikundi chochote.

Wito huo umetolewa leo Oktoba 12, na Mkuu wa Wilaya  ya Ilala, Edward Mpogolo wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) wenye lengo la kupitisha marekebisho ya katiba yao.

Akizungumza na wajumbe wa mkutano huwo, Mpogolo amewatahadharisha viongozi na wajumbe wa Tahliso kutokubali kutumika kwa namna yoyote ili kutimiza malengo la mtu au kikundi.

“Uwepo wa jumuiya hii ya wanafunzi wa vyuo vikuu na kati ni daraja kati ya wanafunzi na viongozi wa serikali  kuu kufikisha changamoto zenu kwa haraka na kutatuliwa,” amesema Mpogolo.

Ameongeza kuwa utulivu wa jumuiya ya hiyo ni hatua kubwa katika elimu zao na kutoa pongezi kwao na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuondoa changamoto za wanafunzi wa vyuo vikuu kwa kutolea mfano wa ongezeko la fedha za kujikimu kutoka kiasi cha 7,000 hadi 10,000 kwa sasa.

SOMA: JK: Wanafunzi wafaidike na tafiti zao

Pia Mpogolo amewaeleza wajumbe hao  misingi ya uongozi, utu na nidhamu ili waweze kutimiza malengo yao kwani kiongozi bora ni yule anayeacha alama na uongozi ni historia.

Aidha, katika mkutano uwo Mpogolo amewataka viongozi wa jumuiya hiyo kuimizana kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kujiandikisha na kupiga kura.

Rais wa Jumuiya ya wanafunzi taasisi za vyuo vikuu Tanzania na kati, Zainabu Kitima amesema kikao hiko cha kikatiba kina lengo la kupitia marekebisho ya katiba ya tahliso ambayo iliandikwa miaka 20 iliyopita.

Hivyo kufanyika kwa marekebisho hayo kutaifanya jumuiya hiyo kufanya kazi kulingana na wakati na mabadiliko ya sekta ya elimu kwa sasa.