Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameuelekeza Wakala ya Barabara (TANROADS) kufunga mizani mitatu inayohamishika (mobile weighbridge) ya kudhibiti uzito wa magari katika eneo la Tunduma ili kuongeza kasi ya upimaji wa magari na kupunguza msongamano wa malori.
Bashungwa ametoa agizo hilo akiwa wilayani Tunduma mkoani Songwe na kueleza kuwa Serikali inatambua changamoto wanayopitia aasafarishaji na wananchi katika eneo hilo kutokana na msongamano wa malori wa muda mrefu na kukwamisha matumzi ya barabara kwa watumiaji wengine.
“Kutokana na changamoto za upimaji wa magari eneo la Mpemba nimeelekeza mizani mitatu ije ikae pale mpemba mmoja ukiharibika wanaweka mwingine ili kuondokana na adha hii ya foleni, nimemuelekeza Meneja wa Tanroads Mkoa Songwe kufikia Jumatano tarehe 20 Novemba 2024 wafunge mzani wa kuhamishika”, amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa ameeleza kuwa serikali inatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa mzani mpya katika eneo la Iboya ili kurahisisha wasafirishaji wanaotoka Zambia kuelekea Mbeya na maeneo mengine ya nchi kupima magari yao bila ya kikwazo chochote.
Aidha, Bashungwa ametoa mwezi mmoja kwa Tanroads Mkoa Songwe kukamilisha ujenzi wa kituo cha maegesho katika eneo la Chimbuya ili kufikia wiki ya kwanza ya mwezi wa Desemba, maegesho hayo yaanze kutumika kwa kupunguza foleni ya malori kukaa barabarani.
Waziri Bashungwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi, Aisha Amour pamoja na Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mohamed Besta ndani ya mwezi mmoja kufanya usanifu utakaowezesha kujenga barabara ya michepuo katika maeneo ya milima mitatu ya Mbalizi, Nyoka na Igawa katika barabara ya Mbeya-Tunduma ambapo magari makubwa na madogo yanapita kwa kupokezana.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo ameeleza kuwa Mkoa tayari umepata eneo la hekari 1,800 kwa ajili ya ujenzi wa bandari kavu katika eneo la Tunduma ili kupunguza changamoto za foleni ya magari ambapo hivi sasa wanaendelea na zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo na Mbunge wa Jimbo la Tunduma, David Silinde amemshukuru Waziri Bashungwa kwa kusikia kilio na kufika kujionea adha ya foleni katika mji wa Tunduma ambapo kwa siku takribani magari makubwa 3,000 yanavuka katika mpaka wa Tanzania na Zambia ambayo ni asilima 72 ya mizigo inayopakuliwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam
Mbunge wa Jimbo la Vwawa, Japhet Hasunga ameiomba serikali kushughulikia changamoto ya msongamano wa malori katika eneo la Tunduma kwani inasababisha ongezeko la gharama kwa wafanyabiashara na Wasafirishaji kutumia muda mrefu barabarani.
0 Comments