SERIKALI imesema kuwa haitamfumbia macho atakayechezea sekta ya mkonge kwa namna yoyote kwani sekta hiyo mtambuka ni ustawi wa maisha ya Watanzania.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Ushirika na Umwagiliaji, Dk. Suleiman Serera  amesema hayo wilayani Korogwe mkoani Tanga wakati akizungumza na viongozi wa Vyama vya Ushirika na Masoko vya Mkonge (AMCOS).

Amesema kuwa serikali inaendelea na mchakato wa kutatua changamoto ya upungufu wa mashine za kuchakata mkonge (korona) ambapo amewahakishia watapatiwa mapema kwani serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inafanya uwekezaji mkubwa katika eneo hilo la sekta ya mkonge.

“Ukizungumzia mkonge Tanga ni maisha, ni siasa, ni kila kitu. Kwa hiyo mtu yeyote atakayecheza na Mkonge amecheza na siasa na maisha ya watu Tanga na sisi hatutaki tuharibikiwe,”amesema Naibu Katibu huyo.

Naye Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Benson Ndiege amezikumbusha AMCOS hizo kujisajili katika programu ya ‘AMCOS to SACCOS’ inayoitaka kila chama cha ushirika wa mazao kiwe na chama cha akiba na mikopo kwa lengo la kuhakikisha wakulima wanapata namna ya kutunza fedha zao wakati wa mavuno na wakati ambao hawana fedha kwa ajili ya kilimo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa wenyeviti wa Amcos hizo tano, Sedrack Lugendo amesema changamoto za wakulima wadogo ni ukosefu wa mashine za kuchakata mkonge wakulima wengi wanakuwa hawachakati mkonge wao kwa wakati ambapo unakuta mtu anakaa hadi mwaka hajachakata zizlizopo hazitoshelezi na ni mbovu