ISRAEL: SERIKALI ya Israel imepanga kukata rufaa kupinga hati ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya kumkamata Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na waziri wa zamani wa ulinzi Yoav Gallant.
Wiki iliyopita, Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu walitoa vibali kwa watu wawili pamoja na kamanda wa kijeshi wa Hamas Mohammed Deif, wakisema kuna sababu za kujiridhisha za kuamini kuwa watu hao watatu waliwajibika kwa uhalifu wa kivita dhidi ya binadamu huko Gaza.
Serikali ya Israel, pamoja na Netanyahu na Gallant wamekanusha vikali dhidi ya shutuma hizo.
Jumatano ya wiki hii, ofisi ya waziri mkuu ilitoa taarifa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu- ICC ya dhamira yao ya kukata rufaa pamoja na kutaka kuzuia utekelezaji wa hati za kukamatwa.
Ofisi ya Netanyahu pia ilisema Seneta wa Marekani Lindsey Graham amesema Bunge la Marekani linaendelea kujadili hati hiyo iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Kiuhalifu ICC kwa lengo la kumkamata Netanyahu na wenzake.
Hatahivyo, Rais wa Marekani Joe Biden alitaja hati hizo zimetolewa kwa lengo la uchochezi.
“Chochote ICC inaweza kumaanisha, hakuna usawa kati ya Israel na Hamas”.
Biden aliongezea,“daima tutasimama na Israel dhidi ya vitisho kwa usalama wake,” alisema Biden.
Nchi wanachama wa ICC, ambazo hazijumuishi Israel wala Marekani , zinalazimika kuchukua hatua katika kumzuia mshtakiwa anayesakwa iwapo atapatikana kuwa katika mamlaka yao.
Baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya zimedokeza kuwa zitaheshimu uamuzi wa ICC, huku nyingine zikikataa.
Serikali ya Uingereza imedokeza kuwa Netanyahu atakamatwa iwapo atasafiri kwenda Uingereza.
0 Comments