MHASIBU Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude amesema wahasibu wana nafasi muhimu katika mnyororo wa uzalishaji wa kiuchumi, hasa katika kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia kama vile matumizi ya akili bandia na kuchangia maendeleo endelevu.
Akizungumza katika mkutano wa mwaka wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania 2024 jijini Dar es Salaam, CPA Mkude ameeleza kuwa sekta ya uhasibu inapaswa kuzingatia maelekezo ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) kuhusu namna ya kuripoti masuala ya mabadiliko ya tabianchi na kutumia fursa zilizopo kuboresha uzalishaji wa kiuchumi.
“Wahasibu ni kiungo muhimu katika mipango na matumizi ya fedha, hasa katika juhudi za Tanzania kufikia uzalishaji wa hewa chafu sifuri ndani ya miaka 50,” amesema CPA Mkude.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA, Prof. CPA Sylvia Temu amesema kongamano hilo lenye muda wa siku tatu lina malengo mawili makuu, likiwemo kubadilishana maarifa na uzoefu wa kitaaluma ili kubaini fursa na changamoto zinazokabili tasnia ya uhasibu.
“Tumejadili uelekeo wa nchi kwa miaka 25 ijayo, ambapo wahasibu wanapaswa kushiriki kikamilifu kubaini fursa za kuendeleza uchumi wa taifa letu na kuleta mchango wenye thamani katika maendeleo ya nchi,” amesema Prof. Temu.
Mwanachama wa heshima wa NBAA, CPA Saimon Sayore, amewataka vijana kuipenda taaluma ya uhasibu, kuitumikia kwa uaminifu, na kuhakikisha wanatunza vyema fedha za taasisi na taifa kwa ujumla.
Kongamano hilo linajumuisha mawasilisho na majadiliano mbalimbali yanayolenga kutoa suluhisho kuhusu mchango wa wahasibu katika kukabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia na kuimarisha maendeleo endelevu.
0 Comments