MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amemtaka mkandarasi anayejenga barabara ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Nne kutoka Maktaba Kuu ya Taifa, Mwenge kuelekea Tegeta hadi Basihaya na kipande cha Mwenge hadi Ubungo kuhakikisha anakamilisha ujenzi huo haraka ili kuboresha usafiri.

Katika kufanikisha hilo, mkandarasi huyo ametakiwa kufanya kazi usiku na mchana.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega katika ziara ya ukaguzi wa mradi huo mapema hii leo, Chalamila amemshauri mkandarasi huyo kuangalia namna ya kuweka huduma za jamii katika vituo vikubwa vya mwendokasi.


“Hivi vituo ukiangalia ni vituo bubu, sasa katika miradi mingine angalieni namna ya kuweka hizi huduma kaeni na sekta binafsi na isiwe hivi vioksi, mnaweza mkaweka hizi ‘malls’ itasaidia watu kupata vocha, choo etc. amesema Chalamila.

Aidha, RC amewaagiza viongozi wa Manispaa ya Kinondoni kuwapa elimu wafanyabiashara waliovamia miundombinu ya barabara ili kupisha miundombinu hiyo.

Mkuu wa Wilaya Kinondoni, Saad Mtambule amesifu kazi kubwa ya Serikali na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) na kuwataka wananchi kuwa wavumilivu kuhusu changamoto za muda mfupi.

Akizungumza msimamizi wa Tanroads, Rajab Idd amesema mradi huo ulianza Novemba 2023 na ulitarajiwa kukamilika April 30, 2025 muda uliotumika ni miezi 14 sawa na 77% na muda uliobaki ni miezi 4 sawa na 23%.

Amesema hatua ya ujenzi iliyofikiwa hadi sasa ni 22% hata hivyo muda uliobaki hautoshi kukamilisha mradi huo na kuomba muda ziada kukamilisha.

Akitoa ufafanuzi mbele ya RC Chalamila, msimamizi huyo amesema zipo changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika kutekeleza mradi huo ikiwemo uwepo wa nguzo za Tanesco, lakini pia kwa kushirikiana na Dawasa na TCCL.

Amesema wanaendelea kuwasiliana na wahusika kuona namna ambavyo wanaweza kuendelea kufanya shughuli zao bila kuathiri huduma zingine za usafiri.

Akipokea maagizo ya Mkuu wa Mkoa, mkandarasi wa mradi Wei kutoka China Geo Engineering Corporation amesema wamepokea maagizo hayo ya kuharakisha mradi huo na kwamba watafanya kazi yenye ubora.