MANYARA: WAZIRI wa nchi ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amewataka wananchi kuchangia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali.
Prof Mkumbo amesema hayo Januari 3,2025 wakati akizindua huduma za kijamii za afya za ujenzi wa miundombinu ya kituo cha afya cha Bassotu Jengo la Mama na Mtoto, jengo la upasuaji, Maabara, nyumba ya kuhifadhia maiti na nyumba ya watumishi.
Pfof Mkumbo alisema wakati serikali inapotoa fedha za maendeleo za kuboresha huduma mbalimbali za afya na elimu wananchi hawana budi kushiriki kwa kuchangia nguvu kazi ili kuhakikisha wanahusika katika utekelezaji wa miradi hiyo.
“Nguvu ya wananchi, ushiriki wa wananchi katika miradi ya maendeleo ni muhimu na pale wanaposhiriki tutambue michango yao” alisema Prof Mkumbo.
Kwa mujibu wa ujenzi wa kituo hicho nguvu za wananchi zilitumika za michango ya milioni 8 kati ya jumla ya gharama ya milioni 408 zilizotolewa na halmashauri katika kukamilisha ujenzi wa kituo hicho cha afya.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Hanang, Mohammedi Kodi alisema baada ya mradi huu kukamilika umepunguza idadi ya akina mama kujifungua nyumbani kutoka wazazi 25 hadi 60 sawa na ongezeko la aslimia 75.
Aidha, upatikanaji wa huduma za afya umechangia kuwapunguzia wananchi gharama na adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hasa za akina mama, wajawazito na watoto.
“Huduma hizo zilikuwa zikipatikana katika hospitali ya wilaya umbali wa KM 55, hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara KM 123 na hospitali ya Haydom iliyoko wilaya ya Mbulu km 25,” alisema Kodi.
Aidha, kituo cha afya cha Bassotu chenye watumishi 17 na kinahudumia wananchi wa vijiji vingine vinne vya Garawja, Mulbadaw, Getunuwas na Bassodesh wapatao elfu 79.
Kwa upande wao wananchi Tito Thomas, Ester Simon na wakazi wengine wa kijiji cha Bassotu wameipongeza serikali ya Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuwasogezea karibu huduma za afya na kuomba kuongezewa huduma za dirisha la matibabu ya wazee.
0 Comments